
BEKI wa kushoto wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Stephano Mwasika anashangazwa na kitendo cha wachezaji wa nafasi kama yake hawafungi mabao.
Mwasika alicheza beki ya kushoto kwa mafanikio katika timu hizo mbili pamoja na Tanzania Prisons ya Mbeya alikoanzia.
“Enzi zetu tulikuwa tunafunga mabao. Unacheza kulinda pembeni lakini wakati huo unaitafutia timu yako ushindi kwa kutafuta nafasi za kufunga mabao na unafanikiwa,” alisema Mwasika.
“Lakini, siku hizi mabeki wa pembeni hawafungi sijui tatizo, au kutofuata maagizo wanayopewa na walimu wao,” alisema.
Msimu ambao Mwasika alifunga mabao mengi ni 2007-2008 ambao Michael Katende raia wa Uganda akiwa Kagera Sugar alikuwa mfungaji.
Mwasika akiwa Tanzania Prisons, alimaliza na mabao saba na kushika nafasi ya nne.
Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’ amesema katika kufunga inategemea na aina ya maagizo anayopewa na benchi la ufundi na kipaji cha mchezaji.
“Kabla ya yote kufunga ni kipaji kwa sababu kuna mabeki wa pembeni wazuri wanapanda juu vizuri lakini wanakosa umakini katika kufunga,” alisema Bares.
“Kufunga ni kipaji tena kwa beki ni kitu kikubwa kwa cha ziada si wote wanaweza kufunga. Ukija kwenye mipango ya mwalimu kuna aina ya mabeki hao wa pembeni wanapewa maagizo ya kucheza maeneo husika. Atembee na mtu fulani, akabe eneo lipi .”
Bares aliwataja mabeki wa pembeni ambao kama watajipanga wanaweza kufunga kitaalamu ni mabeki wa Azam FC, Nicholas Wadada raia wa Uganda na Mzimbabwe Bruce Kangwa wa Simba Mohammed Hussein na Shomari Kapombe, Juma Abdul wa Yanga na Michael Idan wa JKT Ruvu.
No comments:
Post a Comment