
MADRID, HISPANIA . EL Clasico ndo kama ulivyosikia. Lionel Messi na Barcelona yake alikuwa mwepesiii huko Bernabeu, wakati alipokubali kipigo cha mabao Mbili Bila kwenye mchezo wa La Liga kutoka kwa mahasimu wao Real Madrid.
Ushindi huo wa Real Madrid juzi Jumapili mbele ya Barcelona, si kwamba tu umewarudisha Los Blancos kileleni kwenye msimamo wa La Liga, lakini pia umewafanya kushinda mechi nyingi zaidi za El Clasico zinazohusu La Liga. Madrid sasa imeshinda mara 73 moja zaidi ya Barcelona kwenye mechi za El Clasico walizokutana kwenye La Liga. Kuna sare 35 katika mechi za wababe hao.
Kwa ujumla wake, mechi za El Clasico za michuano yote, timu hizo zimekutana mara 192, Los Blancos wakishinda 96.
Ushindi wa juzi, umewafanya Real Madrid wanaongoza kwa kufunga mabao kwenye La Liga, mara 6,152 shukrani kwa mabao Vinicius Junior na Mariano Diaz. Barcelona yenyewe imefunga mabao 6,151. Mchezo huo wa juzi ulimfanya Vinicius kuweka rekodi pia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga kwenye El Clasico katika karne ya 21, akivunja rekodi ya Messi.
Vinicius, 19, amefunga akiwa mdogo kwa siku 26 ukilinganisha na Messi wakati alipofunga kwenye El Clasico, Machi 2007, uwanjani Nou Camp kwenye sare ya 3-3. Lakini, ushindi wa juzi umeweka rekodi nyingine kwa Real Madrid wakipata ushindi wa kwanza nyumbani dhidi ya Barcelona tangu mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment