
Dar es Salaam. Wakati Azam ikipata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting, Mbao imezidi kujiweka katika nafasi finyu ya kubaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Azam ikiwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Never Tigere aliyefunga yote mawili.
Timu hiyo imefikisha pointi 54 katika ligi ikiendelea kubaki katika nafasi ya pili nyuma ya Simba yenye pointi 68.
Simba ina nafasi ya kuongeza pengo la pointi itakapovaana na timu inayoshika mkia Singida United, jijini leo.
Mchezo baina ya Mbeya City na Mbao ulikutanisha timu zinazochuana kuepuka janga la kuteremka daraja msimu ujao.
Mbeya City ikiwa kwenye uwanja wake wa Sokoine, ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mbao matokeo ambayo yameifanya kufikisha pointi 30 na wapinzani wao 22.
Kabla ya mchezo, kocha wa Mbeya City Amri Said ‘Stam’ alisema ni mechi ngumu ambayo watalazimika kucheza kufa au kupona ili kupata pointi tatu.
Amri alisema wanatakiwa kupambana kupata matokeo mazuri katika mechi zote huku akiomba dua baya kwa wapinzani wao walioko katika mstari wa kushuka.
Katika mechi nyingine za jana, Coastal Union iliichapa Lipuli mabao 2-0, Namungo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Biashara United, Ndanda iliilaza Kagera Sugar 2-1, JKT Tanzania ililaza Mwadui 1-0 wakati mchezo baina ya Polisi Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar uliahirishwa kwasababu ya mvua.
No comments:
Post a Comment