
MILAN, ITALIA. STRAIKA, Romelu Lukaku ameanza kujifunza mafunzo ya ukocha kupitia kwenye mtandao wakati huu akiwa amejifungia chumbani kukwepa maambukizi ya virusi vya corona ambavyo ni hatari kwa uhai wa binadamu.
Straika huyo wa Inter Milan ni mmoja kati ya mamilioni ya watu waliolazimika kujifungia vyumbani kutokana na maambukizi ya virusi hivyo vya corona ambavyo vimechukua uhai wa maisha ya wengi duniani.
Lukaku ni moja kati ya wachezaji wa kigeni huko Italia ambao waliruhusiwa kurudi kwenye nchi zao baada ya muda wao wa kuwa karantini kwa siku 14 kumalizika. Italia ni nchi iliyoathiriwa zaidi na virusi hivyo ambavyo vimechukua uhai wa watu zaidi ya 8,200 huku walioambukizwa wanaripotiwa kuzidi 80,000.
Hata hivyo, fowadi huyo wa kimataifa wa Ubelgiji si mchezaji pekee aliyeamua kufanya mafunzo ya ukocha baada ya kiungo wa Borussia Dortmund, Axel Witsel naye kuwa na mpango wa kuanza mafunzo hayo sambamba na supastaa wa Manchester City, Kevin De Bruyne, ambaye amweka wazi dhamira yake ya kuchukua beji ya ukocha daraja la A la B la Uefa ili kuja kufanya kazi ya kuwa kocha baada ya maisha yake uchezaji yatakapofika mwisho.
Kwenye Serie A msimu huu, Lukaku amefunga mabao 17 na kuasisti mara mbili katika dakika 2142 huku akipiga mashuti 55, ambapo 36 kati ya hayo yalilenga magoli ya wapinzani.
No comments:
Post a Comment