
YANGA imeitumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya jana Jumatano kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lipuli, katika uwanja wa Taifa.
Matokeo hayo yameifanya Yanga ifikishe pointi 34 na kuzidi kujiimarisha katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Ufanisi wa mchezaji mmoja mmoja ulikuwa na mchango mkubwa katika kuamua matokeo ya mchezo wa jana na ifuatayo ni tathmini ya jinsi nyota wa timu hizo mbili walivyocheza katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Abubakar Mturo kutoka Mtwara.
Metacha Mnata-6
Hakukutana na changamoto kubwa katika mchezo wa jana kwani kwa muda mrefu Yanga ilikuwa haishambuliwi. Aliwapanga vyema mabeki wake na mara kadhaa aliokoa vyema mashambulizi aliyoelekezewa.
Juma Abdul-9
Alikuwa na mechi nzuri. Alitimiza vyema jukumu la kulinda na alipanda mbele kwa haraka kusaidia mashambulizi kwa kupiga krosi zilizokuwa mwiba langoni mwa Lipuli. Mabao mawili ya ya Yanga yote yaliyokana na krosi zake.
Jafar Mohamed-5
Hakuwa akipanda mbele mara kwa mara na badala yake alijikita zaidi na jukumu la ulinzi ambalo alilitimiza kwa ufasaha kwa muda wote aliokuwa uwanjani.
Said Juma-6
Alifanikiwa kunasa mipira mingi aliyowania na washambuliaji wa Yanga na kuianzisha kwa haraka. Alikuwa na utulivu na alihakikisha anawanyima uhuru Nonga na Saliboko.
Lamine Moro-7
Aliichezesha timu kuanzia nyuma na alitimiza vyema majukumu ya kuilinda timu na alihakikisha anaondosha kila hatari iliyoelekezwa kwenye lango lake.
Papy Tshishimbi-7
Aliilinda vyema safu yake ya ulinzi na kuiunganisha timu kwa pasi zake ambazo nyingi zilienda mbele. Alizunguka uwanja mzima kutafuta mipira na kuisambaza.
Ditram Nchimbi-6
Mikimbio na nguvu zake vilimfanya amuweke katika wakati mgumu beki Paul Ngalema na alikuwa na maamuzi ya haraka kila mpira ulipokuwa miguuni mwake. Alipiga krosi nyingi ambazo kama zingetumiwa vyema na washambuliaji wa Yanga pengine wangeweza kufunga idadi kubwa ya mabao.
Haruna Niyonzima-6
Aliivunja safu ya kiungo ya Lipuli kutokana na uwezo wake wa kutawanya mipira kwa haraka. Alishuka kusaidia timu wakati wapinzani walipokuwa na mpira na pale waliposhambulia alipenyeza mipira ya kutosha kwenda kwa washambuliaji wake.
Yikpe Gnamien-4
Yanga ingeweza kumaliza kazi kipindi cha kwanza ikiwa imefunga takribani mabao matano lakini udhaifu wa Yikpe Gnamien kutumia nafasi alizopata ndani ya eneo la hatari uliwaangusha kwani straika huyo alipoteza nafasi tatu za wazi huku akiwa analitazama lango lakini pia hakuwa tishio sana kwa mabeki wa Lipuli muda wote ambao alicheza.
Mapinduzi Balama-7
Aliwapa shida wachezaji wa Lipuli kutokana na jinsi alivyokuwa akihaha uwanja mzima na kusambaza mipira huku na kule sambamba na kutengeneza nafasi na ndiye alifunga bao la kwanza la Yanga akiunganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdul.
Bernard Morrison-6
Hakuwa ni winga wa kupiga krosi bali muda mwingi alikuwa akiingia ndani kuongeza namba katika ushambuliaji na pia kusimama katika nafasi sahihi na haikushangaza kuona akiifungia Yanga bao la pili kwa kuunganisha vyema krosi ya Juma Abdul
Walioingia
David Molinga-4
Aliangushwa na wenzake ambao walionekana kuchoka katika muda mwingi wa kipindi cha pili ingawa aliwanyima uhuru mabeki wa Lipuli.
Deus Kaseke-3
Alishindwa kutoa msaada kwa beki wake pindi walipokuwa wanashambuliwa na alipiga krosi ambazo hazikuwa na macho.
Ally Sonso-5
Aliisaidia safu ya kiungo ya Yanga kurudi mchezoni baada ya kuzidiwa katika sehemu kubwa ya kipindi cha pili.
DIDA Munishi-7
Kwa nafasi yake alitimiza vyema majukumu kwani aliokoa hatari nyingi ikiwemo zile za ana kwa ana na zile zilizotokana na krosi pia kuipanga safu yake ya ulinzi na mabao yote waliyofungwa hayakutokana na makosa yake.
David Kameta-4
Alionekana kuelemewa na kasi ya mawinga wa Yanga hasa Morrison hali iliyosababisha apaniki na kucheza rafu za mara kwa mara ambazo na kuonyeshwa kadi ya njano. Mabao yote mawili ya Yanga yalitokea upande wake.
Paul Ngalema-5
Kipindi cha kwanza alipata wakati mgumu kumdhibiti Nchimbi na alikuwa anapitwa mara kwa lakini aliimarika katika kipindi cha pili ambacho aliilinda vyema timu na kupanda mbele kusaidia mashambulizi.
Peter Mwangosi-5
Alikosa mawasiliano mazuri na mwenzake David Mwassa katika kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili alitulia na kucheza vyema. Alijitahidi kumdhibiti Yikpe ingawa mara kadhaa alimpa mwanya mshambuliaji huyo kuwashambulia.
David Mwassa-7
Hakuwa katika nafasi sahihi kwa mabao yote mawili ya mwanzo ya Yanga na aliruhusu krosi zipite juu yake ingawa baadaye aliimarika na kuokoa hatari nyingi ambazo zilielekezwa langoni mwa Lipuli. Faulo yake aliyopiga kwa ustadi katika dakika ya 58 ndio iliipatia timu yake bao.
Novart Lufunga-6
Mara kwa mara aliachia mianya ambayo Yanga waliitumia kupenyeza mipira kwenda katika eneo lao la hatari na kujikuta wakishambuliwa lakini baadaye alijirekebisha na kuilinda vyema safu yake ya ulinzi.
Said Mussa-5
Alipoteza mipira mara kwa mara na alionekana kuwa mbinafsi kwa kuchelewa kutoa mpira pale ulipokuwa mguuni. Aliwapa wakati mgumu mabeki wake wa pembeni kwa kutoshuka kuwapa msaada pale walipokuwa wanashambuliwa.
Fredy Tangalu-6
Muda mrefu wa mchezo alishindwa kuiunganisha vyema timu kwani pasi zake zilipotea ingawa baadaye alirudi mchezoni na kuipeleka mbele timu.
Paul Nonga-7
Hakupata huduma nzuri kutoka kwa viungo wa Lipuli lakini alipambana kusaka mipira ambayo aliitunza vyema na kuwapa mwanya wenzake kusogea. Alitengeneza nafasi kadhaa ambazo zingetumiwa vyema timu yake ingeweza kufunga zaidi ya bao moja.
Daruwesh Saliboko-5
Alishindwa kufurukuta mbele ya mabeki wa Yanga na alikosa shabaha kwa nafasi chache alizopata.
Kenneth Masumbuko-8
Alijitolea dakika zote. Pasi zake na uwezo wake wa kupiga chenga viliwaweka katika wakati mgumu walinzi wa Yanga.
Walioingia
Shaaban Ada-5
Aliongeza uimara wa Lipuli katika safuya kiungo na kuiongezea kasi timu katika kipindi cha pili.
No comments:
Post a Comment