
BARCELONA, HISPANIA . KATIKA miaka ya karibuni Lionel Messi amekuwa akitawala tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, akishinda mara tatu mfululizo.
Lakini, msimu huu mambo yanaonekana kubadilika na kuna kila dalili za kupatikana kwa mfalme mpya wa ufungaji barani Ulaya kutokana na kuwa Messi yuko nyuma ya Ciro Immobile anayeongoza mbio hizo kwa tofauti ya mabao 12, akiwa amefunga mabao 14 tu katika msimu huu wa La Liga.
Tuzo hiyo huenda kwa mchezaji mwenye pointi nyingi ambazo hizo hupatikana kwa kuzidisha kwa idadi ya mabao, ambapo ligi kubwa kila bao lina pointi 2, huku ligi nyingine bao lina pointi 1.5 na kuna ligi bao moja pointi 1.
Hadi sasa tano bora ya kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya imes
imama kama ifuatavyo.
5. Erling Haaland (Mabao 24, Pointi 40)
Borussia Dortmund ilimsajili wakati wa dirisha dogo la Januari kutokea RB Salzburg, ambako alikuwa amefunga mabao 16, na tangu atue Signal Iduna Park amefunga manane.
Licha ya kuwa na mabao 24, lakini bado ana pointi 40 kwa sababu mabao 16 aliyofunga Austria yanazidishwa mara 1.5 hivyo kupata pointi 24, wakati yale nane ya Bundesliga yanazidishwa mara 2 na kupata pointi 16, ambapo zikijumlishwa zinapatikana pointi 40.
4. Cristiano Ronaldo (Mabao 20, Pointi 40)
Staa huyu wa Juventus amewahi kutwaa tuzo hii mara nne - mara moja alifanya hivyo baada ya kufunga mabao 31 akiwa na Manchester United, lakini mara nyingine tatu alifanya hivyo akiwa na Real Madrid.
Mkongwe huyo amekuwa na kiwango bora katika mwaka 2020 ambapo amefunga mabao 15 katika mechi 10 akiwa na kikosi cha Juventus kilicho chini ya Maurizio Sarri, kwa ujumla msimu huu amefunga mabao 20 sawa na pointi 40.
3. Timo Werner (Mabao 20, Pointi 40)
Kiwango cha Mjerumani huyu msimu huu kimezivuta klabu za Liverpool na Chelsea kuisaka saini na tayari amefunga mabao 20 katika mechi 22 za Bundesliga akiwa na RB Leipzig.
Kama ilivyo kwa Serie A, Bundesliga nayo bao moja lina pointi 2, hivyo kwa mabao yake 20 aliyofunga ana pointi 40, 12 nyuma ya Immobile anayeongoza mbio hizo.
2. Robert Lewandowski (Mabao 23, Pointi 46)
Straika huyu wa kimataifa wa Poland yuko nyuma ya kinara wa mbio hizi kwa tofauti ya mabao matatu ambayo ni sawa na pointi sita.
Akiwa na miaka 31, Robert Lewandowski ameendelea kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Bayern Munich na kila msimu amekuwa akifunga mabao mengi kwenye Bundesliga. Lakini bado hajawahi kutwaa tuzo hii kama Immobile.
1. Ciro Immobile (Mabao 26, Pointi 52)
Straika huyu wa Lazio ndiye anayeongoza orodha hii ya kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya akiwa na mabao 26 katika mechi 24 za Ligi Kuu ya Italia.
Kiwango cha straika huyo kimeisaidia Lazio kupambana na vinara Inter Milan na Juventus katika mbio za ubingwa wa Serie A. Lazio wako nyuma ya Juventus kwa tofauti ya pointi moja. Kutokana na idadi hii ya mabao Immobile kwa sasa ana jumla ya pointi 56, kwa sababu goli moja la Serie A lina pointi 2 na ana nafasi kubwa sana ya kutwaa kiatu hicho msimu huu.
No comments:
Post a Comment