MADRID, HISPANIA . DIRISHA dogo la usajili la Januari linafungwa kesho huku kila timu ikiimarisha kikosi chake kulingana na mahitaji yake ili kumalizia nusu ya pili ya msimu huu wa 2019-20.
Lakini, wakati ikiwa imesalia siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili la Januari, Mwanaspoti linakupa klabu tano zinazoongoza kumwaga Pesa katika usajili tangu 1999-2000 hadi leo hii.
5. JUVENTUS
IDADI: Wachezaji 830
GHARAMA: Euro 1.92 bilioni
MCHEZAJI GHALI: Cristiano Ronaldo
BEI: Euro 104.3 milioni
Moja ya sifa kubwa ambayo Juventus imejijengea katika miaka ya karibuni ni kuwanasa bure mastaa wenye majina makubwa kama akina Aaron Ramsey, Paul Pogba, Adrien Rabiot, Dani Alves, Andrea Pirlo, Luca Toni na wengine wengi kibao walitua Turin bure kabisa, lakini pia linapokuja suala la kutumia Pesa, Juventus wako vizuri tangu msimu wa 1999-2000, wametumia Euro 1.92 bilioni kusajili wachezaji 830 huku usajili wa Ronaldo kutoka Real Madrid ndiyo wa pesa ndefu, Euro 104.3 milioni.
4. BARCELONA
IDADI: wachezaji 248
GHARAMA: Euro 2.02 bilioni
MCHEZAJI GHALI: Antoine Griezmann
BEI: Euro 126.8 milioni
La Masia ndiyo sehemu ambayo Barcelona inazalisha wachezaji wake, huku wengi wakipandishwa kikosi cha kwanza na kucheza kwa mafanikio. Kina Andres Iniesta, Xavi Hernandez, Sergio Busquets, Lionel Messi na wengine wengi ni zao lao, lakini mbali na kuzalisha wachezaji, wakati mwingine Barca huingia sokoni kusajili mastaa kwa pesa ndefu. Barca imetumia jumla ya Euro 2.02 bilioni kusajili wachezaji 248, Antoine Griezmann ndiyo ghali zaidi akitua Nou Camp kwa Euro 126.8 milioni.
3. MANCHESTER CITY
IDADI: Wachezaji 493
GHARAMA: Euro 2.05 Bilioni
MCHEZAJI GHALI: Kevin De Bruyne
BEI: Euro 65.1 milioni
Awali, Man City ilikuwa timu ya kawaida sana na haikuwa na nguvu kubwa sokoni, lakini tangu Sheikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan alipoinunua Septemba 2008, imekuwa tishio huku mmiliki huyo akitumia Pesa kibao kuibadilisha kutoka kuwa timu ya kawaida inayopambana kukwepa kushuka daraja hadi kutwaa ubingwa wa England na kutawala soka la nchi hiyo. City imesajili wachezaji 493 kwa Euro 2.05 bilioni na Kevin De Bruyne ndiye ghali zaidi kutua Etihad akisajiliwa kwa Euro 65.1 milioni kutoka VfL Wolfsburg.
2. CHALSEA
IDADI: Wachezaji 531
GHARAMA: Euro 2.09 bilioni
MCHEZAJI GHALI: Kepa
BEI: Euro 84.8 milioni
Kabla Roman Abramovich hajaichukua Chelsea ilikuwa bora, lakini haikuwa na nguvu za kuwania ubingwa, lakini chini ya utawala wake bilionea huyo wa Kirusi ametumia pesa ndefu kuifanya kuwa tishio England na Ulaya. Tangu msimu wa 1999 – 2000 hadi leo Chelsea imetumia Euro 2.09 bilioni kusajili wachezaji 531, huku kipa, Kepa Arrizabalaga akisajiliwa kwa pesa ndefu zaidi akitua kwa Euro 84.8 milioni akitokea Athletic Bilbao.
1. REAL MADRID
IDADI: Wachezaji 265
GHARAMA: Euro 2.22 bilioni
MCHEZAJI GHALI: Eden Hazard
BEI: Euro 105.5 milioni
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ni muasisi wa sera ya Galacticos pale Santiago Bernabeu, chini ya sera hii klabu hiyo hutumia pesa kubwa kutengeneza vikosi vya wachezaji mastaa. Enzi za kina Zinedine Zidane, Luis Figo, David Beckham, Michael Owen, Ronaldo de Lima kisha akina Gareth Bale, Cristiano Ronaldo, Kaka, Karim Benzema, James Rodriguez na wengine kibao, sera hii ndiyo sababu ya Madrid kuongoza orodha hii kutokana na kutumia jumla ya Euro 2.22 bilioni katika kipindi cha miaka 20, huku ikisajili wachezaji 265 na Eden Hazard ndiyo mchezaji ghali zaidi akitua Bernabeu kwa dau la Euro 105.5 milioni akitokea Chelsea.
No comments:
Post a Comment