
LIVERPOOL, ENGLAND . JURGEN Klopp amewashtua watu baada ya kusema kuwa hatakuwa kwenye benchi kuiongoza Liverpool katika mchezo wa marudiano wa Kombe la FA dhidi ya Shrewsbury Town katika Uwanja wa Anfield, Februari mwaka huu.
Sare ya mabao 2-2 imemaanisha kuwa Liverpool na Shrewsbury, zitarudia Februari mwaka huu kipindi ambacho timu zingine zitakuwa kwenye mapumziko ya majira ya baridi na Klopp sasa ameibuka na kusema kuwa kikosi chake cha kwanza hakitacheza mechi hiyo kwa sababu wachezaji watakuwa mapumzikoni na badala yake kikosi cha vijana chini ya miaka 23, chini ya kocha Neil Critchley ndiyo kitaiwakilisha timu hiyo Anfield.
Klopp hatakuwa kocha wa kwanza na haitakuwa mara yake ya kwanza kutokaa kwenye benchi la timu yake kwenye mechi. Hawa hapa makocha watano waliowahi kufanya hivyo hapo awali.
Sam Allardyce
Allardyce hakuwa kipenzi cha mashabiki tangu alipoteuliwa kuinoa Everton akichukua nafasi ya Ronald Koeman, Novemba 2017, na kocha huyo alizidi kuchukiwa na mashabiki baada ya kuamua kutuma kikosi cha pili katika mechi ya Europa League dhidi ya Apollon Limassol, nchi Cyprus huku yeye akibaki England na kikosi cha kwanza akijiandaa na pambano dhidi ya Liverpool. Mechi hiyo ilikuwa ya mwisho ya Everton katika hatua ya makundi na hawakuwa na nafasi ya kusonga mbele, kutokana na kufungwa mara nne na kutoka sare mara moja katika mechi tano za kwanza.
Baada ya kelele nyingi ikatangazwa kuwa Allardyce hakusafiri na timu kwa sababu alikuwa anatakiwa kukutana na daktari wake, lakini katika mchezo huo Craig Shakespeare na Duncan Ferguson waliiongoza Everton kushinda kwa mabao 3-0, huku Everton ikifanikiwa kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool, Anfield mwisho wa wiki hiyo.
Neil Warnock
Mashabiki wa Leeds hawakuwa wanamkubali Warnock na moja ya sababu za kumchukia ni kitendo cha kutumia muda mwingi sana katika mji wa Cornwall kabla ya kukosa mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Birmingham City kutokana na ugonjwa. Warnock alisikiliza mechi hiyo redioni, huku akimpigia msaidizi wake Mick Jones kumtaka afanye mabadiliko mawili wakati wa mapumziko muda huo timu yake ilikuwa nyuma kwa bao 1-0.
Jones aliamua kuongoza kwa sauti ili wachezaji wote wasikie maelekezo ya bosi wao kwenye simu na uamuzi wa kumuingiza Luciano Becchio ulizaa matunda kwa sababu alisawazisha bao na kufanya mchezo huo kwenda katika marudiano na Leeds kushinda 2-1.
Edgar Davids
Huwa inasahaulika kuwa Davids alianza vizuri maisha yake katika kikosi cha Barnet akiwa kama kocha mchezaji, lakini timu hiyo ilishuka daraja mwisho wa msimu.
Tangu mwanzo ilikuwa inaaminika kuwa Davids hatakaa kwa muda mrefu kwenye timu hiyo ambayo alijipa jezi namba moja, akipewa kadi nyekundu mara tatu katika mechi tano huku akikubaliana na wamiliki wa timu hiyo kuwa hatasafiri na timu kwenye mechi za ugenini ambazo zitawalazimu walale huko na kumuachia msaidizi wake Ulrich Landvreugd aongoze timu.
Sir Alex Ferguson
Aliiongoza Manchester United kwenye jumla ya mechi 1,500 huku akikosekana kwenye benchi mara tatu tu, mara ya kwanza alienda kwenye msiba wa mke wa kaka yake, kisha akakosa mechi dhidi ya Manchester City, Novemba 2000 kwa sababu alienda kuhudhuria harusi ya mtoto wake nchini Afrika Kusini. Fergie aliikosa mechi hiyo kwa sababu awali wakati wanapanga tarehe ya harusi ambapo waliamini Novemba 18 itakuwa ina mechi za kimataifa, lakini baadaye ratiba ikabadilika na tarehe ya harusi ikiwa imeshapangwa.
Anadai alilazimika kuangalia mechi hiyo kwenye televisheni huku msaidizi wake Steve McClaren akikaa kwenye benchi kuiongoza United kushinda bao 1-0 lililofungwa na David Beckham. Mechi ya tatu Ferguson kuikosa ilikuwa Septemba 2010, aliamua kuipotezea mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Scunthorpe United ambayo timu yake ilishinda 5-2, awali iliripotiwa kuwa Fergie alikosa mechi hiyo kwa sababu alienda kuwaangalia Valencia aliyotakiwa kukutana nayo wiki moja baadaye kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini baadaye mmoja kati ya wasaidizi wa Fergie, Eric Steele alitoboa siri kuwa kocha huyo hakwenda Hispania kuiangalia Valencia ilikuwa inacheza na Atletico Madrid, badala yake alikuwa anataka kumtaza kipa kinda David de Gea aliyekuwa kwenye lango la Atletico.
Jurgen Klopp
Desemba mwaka jana wakati timu hiyo ikiwa nchini Qatar ikishiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu kikosi cha vijana kililazimika kucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Aston Villa.
No comments:
Post a Comment