
London, England. Pep Guardiola amesema Manchester City ina kazi mbele yake licha ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester United.
Man City ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Old Trafford iliiduwaza Man United katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ligi.
Timu hiyo imelipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa mwezi uliopita.
Marcus Rashford wa Man United alifunga bao dakika ya 70 akitanguliwa na mabao matatu ya Bernardo Silva, Riyad Mahrez kabla ya Andreas Pereira kujifunga.
Mabeki wa kati wa Man United, Phil Jones na Victor Lindelof walicheza chini ya kiwango kwa kuruhusu mashambulizi langoni mwao.
Nyota wa zamani wa Man United Darren Fletcher alisema ni mabeki dhaifu wa kati ambao amewaona katika kikosi hicho.
Guardiola alisema ana amini mchezo wa marudiano utakuwa na upinzani kwa kuwa Man United si timu ya kubeza licha ya kuifunga idadi kubwa ya mabao.
“Tulicheza kwa kiwango bora kipindi cha kwanza. Huwezi kutarajia kwamba ukija hapa utapata mabao manne au matano ndani ya dakika 45, lakini 3-0 inatosha,”alisema Guardiola.
Kocha wa Man United, Ole Gunner Solskjaer alisema bao la pili liliwavuruga wachezaji wake na dakika 45 za kipindi cha pili walishindwa kuhimili kasi ya Man City.
“Bao la kwanza halikuwa na madhara tuliendelea kusimama imara, bao la pili lilianza kutuvunja nguvu na lilipoingia la tatu tulipoteza mwelekeo,”alisema Solskjaer.
Hii ni mara ya kwana Man United kufungwa mabao matatu kwenye uwanja wake tangu mwaka Mei 1997 ilipopoteza dhidi ya Middlesbrough.
No comments:
Post a Comment