Search This Blog

Monday, December 23, 2019

TFF yawakuna wadau hapa tu!

JUMAMOSI iliyopita, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) lilifanya mkutano mkuu wa mwaka jijini Dar es Salaam na kuridhia mabadiliko ya katiba kwa baadhi ya mambo ambayo waliona yana umuhimu.

Uamuzi wa TFF kupunguza kanda za wawakilishi wa timu kutoka 13 mpaka sita, yamepongezwa na wadau wa soka nchini kwamba utasaidia kupunguza gharama ambazo hazikuwa za msingi.

Kutokana na kupunguzwa kwa kanda hizo, sasa wajumbe wa mkutano mkuu watabaki 85 kutoka 130.

Pia, mabadiliko mengine ya katiba hiyo ni kuondoa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa wa kuchaguliwa na sasa atateuliwa na Rais.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, walisema mabadiliko hayo yakitekelezwa yatasaidia kuleta maendeleo ya soka nchini.

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema mkutano huo ulikuwa na tija ingawa kuna maeneo aliyaona yanahitaji elimu ya kuboresha.

Advertisement

Alisema TFF imekuwa ikihaha kupata pesa za kuendesha shirikisho hilo, hivyo kubakiza kanda sita kutoka 13 anaona itasaidia kupunguza gharama ambazo hazikuwa na msingi.

“Vikao vya kamati vina gharama kubwa sana bora hizo kanda zipungue ili kuongeza tija kwenye maendeleo ya soka letu, hilo nimelifurahia na kulipongeza.

“Mabadiliko ya makatibu wa mikoa kuwa wasimamizi wa ligi kwa maana ya kuandika ripoti na mengineyo pia ni zuri. Awali ilikuwa ni kazi ya wajumbe, jambo ambalo nilikuwa naona umakini unakuwa mdogo kusimamia sehemu nyingi mtu mmoja,” alisema Mayay.

Jambo aliloliona linapaswa kuboreshwa ni kutolewa elimu ni la uhusishwaji wa vyama vyote vya soka ili uamuzi ukitolewa unakuwa wa pande zote.

“Vyama kama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza), Chama cha Waamuzi (Frat), Chama cha Madaktari wa Michezo (Tasma), Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) na Chama cha Makocha (Tafca), lazima viwepo kwa lengo ya kutoa uamuzi wa pamoja ili asiwepo wa kulalamika,” alisema.

Mwenyekiti Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MRFA), Elias Mwanjala alisema ingawa mabadiliko yanaonekana kugusa ngazi za juu, anaamini yataanza kuonekana taratibu kwenye ngazi za chini.

“Ni mabadiliko mazuri, mfano makatibu nao wataanza kulipwa mishahara, ingawa matunda yake hayawezi kuonekana kwa haraka ila ipo siku umuhimu wake utakuwa wazi,” alisema.

Mwenyekiti wa KMC, Herry Nassor Misinga alisema kwa namna alivyoona mabadiliko yaliyotangazwa kwenye mkutano huo anaona neema ya mafanikio ya soka huko mbele.

“Mfano nilifurahishwa na kipengele cha kupunguza wajumbe wakati mwingine mlundikano wa watu unakuwa hauna tija. Kinachotakiwa ni uzito wa uamuzi kwa faida ya soka, pia itapunguza gharama,” alisema.

Naye Katibu wa Tanzania Prisons, Ajabu Kifukwe alisema amefurahia kupunguzwa kwa wajumbe ambao walikuwa wanawakilisha timu zao, kwamba hakuwahi kuona faida yao.

“Sijawahi kuwaona hao wawakilishi wetu wakaja kutuuliza kwamba wanataka watuwakilishe nini, tunasikia tu wamekwenda kwenye vikao, hapo wanamwakilisha nani? Nimefurahi sana walivyopunguzwa,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Almasi Kasongo alisema kwa uzoefu wake wa uongozi hakuwahi kuhudhuria mkutano mkuu wa TFF mzuri na ulioendeshwa kwa kifupi kisha ukawa na tija kama huu wa sasa.

“Binafasi naona wamechelewa kufanya mabadiliko hayo, hili ndilo soka la kisasa linavyotakiwa, mkutano ulikuwa mzuri na umefanyika muda mfupi, vitu vilivyojadiliwa ni vya msingi sana.

“TFF inaundwa na vyama vya soka vya mikoa, sasa tunapaswa kujitathimini namna ya kutekeleza ajenda zilizotolewa kwenye mkutano huo, hilo ndilo ninaloliona la msingi kwangu,”alisema.

Kasongo aliweka wazi kati ya mambo ambayo ataanza nayo DRFA ni kuhakikisha kozi za makocha, waamuzi zinafanyika kwa wakati, kuwa na timu za vijana.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...