
Kocha wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Francis Kimanzi amedai kuwa mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa mashindano ya Chalenji hauna tija na unachangia kudumaa kwa soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kimanzi ambaye timu yake imemaliza katika nafasi ya tatu ya mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) alisema kuwa iko haja kwa baraza hilo kuyatazama na kutafuta namna mpya ya kuyafanya yawe chachu ya kuinua soka badala ya kudidimiza.
“Wakati mwingine tunatakiwa tuwe wakweli ili tuweze kusaidia soka letu kupiga hatua. Ratiba ya haya mashindano sio rafiki kwani mara kwa mara yanachezwa katika kipindi ambacho ligi inaendelea hivyo klabu nyingi zinakuwa haziko tayari kuwaachia nyota wake zikihofia kuwa wanaweza kupata majeruhi.
Sisi kwa mfano tumekuja hapa tukiwa hatujapata muda wa kukaa na wachezaji na kuwaandaa badala yake nikalazimika kufanya hivyo tukiwa huku na bado tukapewa kiwanja kidogo cha mazoezi ambacho hakimpi nafasi kocha kuandaa wachezaji,” alisema Kimanzi.
Kimanzi alisema kuwa kitendo cha kucheza mechi mfululizo bila kupata muda wa kupumzika na aina ya uwanja uliotumika vinawanyima fursa wachezaji kuonyesha na kuthibitisha uwezo na ubora wao.
“Unacheza mechi siku moja, unapumzika siku moja na keshokutwa yake unaingia tena uwanjani kucheza mechi sasa hapo miili ya wachezaji inakuwa haijapumzishwa na inakuwa ni vigumu kwao kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo unaofuata.
Lakini pia tunatumia uwanja wenye nyasi bandia ambao umekuwa ukiwaumiza wachezaji hasa unapotumika kwa mechi za kwanza mchana hasa jua linapowaka jambo ambalo linawaumiza wachezaji kwani joto linakuwa kali na wanakuwa wanakimbia au kutembea uwanjani wakiwa kama wanavutwa na ‘bigijii’
Sasa mbaya zaidi, wachezaji wanapumzika kwa muda mfupi hivyo wanakuwa wamechoka halafu bado unaambiwa namba ya wachezaji inayohitajika ni 20. Sasa kwa idadi hiyo kocha unakuwa hauna wigo mpana wa upangaji wa kikosi,” alisema Kimanzi.
Kocha huyo alisema imefika hatua idadi kubwa ya timu zimekuwa zikishiriki ili kuondoa lawama jambo ambalo linafanya mashindano yakose mvuto na ushindani wa kweli
No comments:
Post a Comment