
MANCHESTER, ENGLAND . STAA wa Red Bull Salzburg, Erling Haaland amewapa matumaini mashabiki wa Manchester United kuhusu dili la kutua huko Old Trafford kwa mkwanja wa Pauni 76 milioni.
Haaland, mtoto wa staa wa zamani wa Leeds United na Manchester City, Alf-Inge, amefunga mabao 28 katika mechi 22 za michuano yote aliyocheza msimu huu na amepiga hat-trick tano, ikiwamo moja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kiwango chake bora cha msimu huu kimezivutia timu kibao vigogo kutaka huduma yake wakiwamo Man United ambao wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumchukua staa huyo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa Januari.
Juzi Jumanne iliripotiwa kwamba Man United inakaribia kukamilisha dili la Pauni 76 milioni la kumnasa straika huyo, Haaland - lakini watambakiza kwa mkopo kwenye timu yake ya Red Bull Salzburg hadi mwishoni mwa msimu.
Staa huyo aliwapagawisha zaidi mashabiki wa timu hiyo baada ya kutuma picha yake kwenye mitano ya kijamii ikimwonyesha akisaini jezi ya Man United inayotumika kwa msimu huu wa 2019/20. Haaland alituma picha hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Lakini, staa huyo alikuja kuwavuruga zaidi mashabiki wa Man United baada ya kutuma picha nyingine zinazomwonyesha akiwa anasaini jezi za Napoli na Leeds United na kushindwa kuwaaminisha kama kweli anakwenda kutua Old Trafford.
Taarifa za hivi karibuni zilidai mchezaji mwenyewe anataka kwenda Man United. Timu nyingine zinazomtaka mshambuliaji huyo ni Red Bull Leipzig na Borussia Dortmund. Haaland aliwahi kufanyakazi chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer huko Molde na sasa anataka waungane tena Old Trafford.
No comments:
Post a Comment