
London, England. Mikel Arteta anatarajiwa kutangazwa rasmi kocha mpya wa Arsenal baada ya kufikia makubaliano ya kutia saini mkataba wa miaka mitatu na nusu.
Lakini Pep Guardiola alisema Arteta atakuwa na kazi ngumu ya kuisuka upya Arsenal kwa kuwa ni klabu kubwa duniani.
Kocha huyo wa Manchester City alisema Arsenal imeyumba tangu alipoondoka Arsene Wenger, hivyo Arteta atakuwa na kazi kubwa ya kurejesha matumaini kwa wadau wa klabu hiyo.
“Klabu inataka kufanya mabadiliko ya kocha inakuwa na matumaini anayekuja anapaswa kuwa bora zaidi. Arsenal ni timu bora kwa zaidi ya miaka 20,”alisema Guardiola.
Hata hivyo, alisema Arteta ni kocha sahihi Arsenal kwa kuwa katika kipindi alipokuwa msaidizi wake Man City alifanya kazi nzuri na amemtakia kila la kheri.
Arteta anakwenda kujaza nafasi ya Unai Emery aliyefukuzwa baada ya kupata matokeo mabaya katika mechi za Ligi Kuu England msimu huu.
Nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo alifikia makubaliano hayo jana na bosi wa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo Josh Kroenke ambaye muda mfupi baada ya kufikia mwafaka alipanda ndege kwenda Marekani.
Kibarua cha kwanza kwa Arteta kitakuwa katika mchezo wa Ligi Kuu ambao Arsenal itavaana na Everton Jumamosi wiki hii.
Idadi kubwa ya wachezaji nguli wa zamani wa timu hiyo akiwemo mchambuzi wa soka Martin Kaown wameonyesha matumaini kwa kocha huyo kijana mwenye miaka 37.
Ingawa hana uzeofu wa kutosha kwa nafasi ya kocha mkuu, Arteta alishinikiza kulipwa mshahara mzuri unaokadirikia kufikia ule wa Emery ambapo atavuna Pauni5 milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, Arteta anapaswa kuwa na benchi la ufundi lenye uzoefu wa kutosha ambalo litakuwa chachu yake ya kufanya vyema Arsenal.
No comments:
Post a Comment