Search This Blog
Sunday, September 15, 2019
Waziri Kalemani amtumbua Meneja wa TANESCO
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumwondolea wadhifa wake, aliyekuwa Meneja wa shirika hilo wilayani Bukombe, Thadei Mapunda kutokana na utendaji kazi usioridhisha na kuteua Meneja mwingine.
Alitoa maelekezo hayo, akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo.
“Mkurugenzi Mtendaji Makao Makuu, sijaridhishwa na utendaji kazi wa Meneja wa Wilaya hii. Naagiza muweke pembeni sasa hivi. Huyu siyo Meneja wa hapa kuanzia leo,” alielekeza Waziri.
Akizungumza na wananchi wa Bukombe, katika uwanja wa stendi ya zamani, Waziri Kalemani aliwaeleza kuwa uamuzi wake wa kumwondoa Meneja huyo unatokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa maeneo mbalimbali wilayani humo kutokupatiwa huduma ya umeme pasipo sababu za msingi.
“Nimepita Kapela, kuna nyumba nzuri, kubwa lakini hazina umeme. Ni masikitiko makubwa sana, Halafu namuuliza Meneja hizi nguzo zimechimbiwa lini; ananiambia mwezi uliopita wakati nauona ni udongo wa leo na jana.”
Katika hatua nyingine, Waziri alisisitiza kuwa gharama za kuunganishiwa umeme vijijini ni shilingi 27,000 na kuwaonya mameneja wa TANESCO nchi nzima kutowalipisha nguzo wananchi vijijini.
Aidha, kabla ya kwenda kuzungumza na wananchi hao, Waziri alipita maeneo mbalimbali kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, ambayo ni pamoja na soko kuu na kuagiza pafungwe transfoma na maduka yaliyopo eneo hilo yaunganishiwe umeme ndani ya siku moja.
Vilevile, Waziri alitoa siku 30 kwa mameneja wa TANESCO wa Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa, kwa kushirikiana na mkandarasi, kuhakikisha maeneo ya Nifa, Majengo, Kerezia, Maghorofani, Stendi Kuu na Stendi ya Mabasi yawe yamewashiwa umeme ifikapo mwisho wa mwezi huu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, alimshukuru na kumpongeza Waziri Kalemani kwa kazi kubwa anayoifanya.
“Ninao ujasiri na imani kwamba, chini ya Dkt Kalemani, wananchi wa Bukombe, maswali yenu ya umeme yamepata majibu leo,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Mkumba, pamoja na kumpongeza Waziri Kalemani na Mbunge wa eneo husika Doto Biteko kwa kuchukua hatua za kushughulikia matatizo ya umeme kwa wananchi husika mapema; aliahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Punguza kilo tano kwa siku saba
NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...
-
Kiwanja kinauzwa kipo Dodoma Mahungu njia ya kwenda Singida kabala hujafika NALA. Kiwanja ni cha Makazi kinaukubwa wa Sqm 450 ( 15 X...
-
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Kai...

No comments:
Post a Comment