Search This Blog

Tuesday, August 20, 2019

Waziri Kabudi afungua rasmi kikao kazi maalum cha Mabalozi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amewataka Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje kuongeza jitihada katika kuhamasisha wawekezaji, wafanyabiashara na watalii kuja nchini ikiwa ni utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Waziri Kabudi ameyasema hayo tarehe 20 Agosti 2019 wakati akifungua rasmi  kikao kazi maalum cha Mabalozi kinachofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 20 hadi  23 Agosti 2019.

Waziri Kabudi alisema kuwa, Mabalozi ambao wana jukumu kubwa la kusimamia maslahi ya Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani, wameendelea kufanya kazi nzuri katika  kuhakikisha dhana ya diplomasia ya uchumi inafikiwa na kwamba matokeo ya jitihada hizo ni pamoja na kuongezeka kwa watalii, wawekezaji na wafanyabiashara nchini. Pia kumekuwa na ongezeko la fursa za ufadhili wa masomo na ajira kwa Watanzania kwenye nchi mbalimbali.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kukutana nanyi Waheshimiwa Mabalozi tangu niteuliwe na Mhe. Rais kwenye wadhifa huu. Nazipongeza jitihada zenu katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwani matokeo tunayaona kwa biashara kuongezeka hapa nchini watalii na hata wawekezaji. Hivyo nataka mwongeze jitihada zaidi ili nchi yetu ifikie azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025” alisema Kabudi”.

Aidha, Waziri Kabudi alitoa rai kwa Mabalozi kuendelea kuwahamasisha Watanzania waishio nje (Diaspora) kujiandikisha na kuanzisha jumuiya zao ili kwa namna moja au nyingine na wao washiriki kuchangia maendeleo hapa nchini.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili Mabalozi hao ikiwa ni pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo ya balozi, Kabudi alieleza kuwa Wizara inaendelea kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi, Kiongozi wa Mabalozi hao,  Naimi Aziz, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo Mabalozi walipata fursa ya kuitembelea. Alisema kuwa, miradi hiyo ni chachu ya maendeleo katika kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati. Tumepata fursa ya kuiona miradi hiyo ikiwemo ile ya ujenzi wa barabara, reli na umeme. Kimsingi miradi hii inalenga kumwondolea umaskini Mtanzania kwa vile pamoja na mambo mengine itarahisha usafirishaji na kumwezesha mkulima kusafirisha kwa urahisi mazao yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kupitia miundombinu hiyo”, alisema Balozi Aziz.

Pia aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuandaa na kufanikisha Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanyika nchini kwa mafaniko makubwa.




No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...