Search This Blog
Thursday, August 8, 2019
Serikali kula sahani moja na watakaohujumu Ushirika
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza watendaji wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu katika vyama vya ushirika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wote wa ushirika nchini wahakikishe wanaongoza vyama vya ushirika kwa kufuata Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013, kanuni na taratibu zilizopo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nane nane Kitaifa kwenye viwanja vya maonesho Nyakabindi mkoani Simiyu kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa Wanaushirika wote nchini kuhakikisha wanachagua viongozi wenye weledi, wachapakazi, waadilifu na wanao upenda ushirika ili ushirika uimarike na kuwa endelevu.
Amesema historia inaonesha kwamba miaka ya nyuma ushirika ulifanya kazi nzuri katika kusimamia uzalishaji, tija, uchakataji na masoko ya mazao. “Hata hivyo, ushirika ulianza kulegalega katika miaka ya 1980”.
Waziri Mkuu amesema kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuanzisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika kama chombo cha kusimamia shughuli za maendeleo ya ushirika nchini.
Amesema katika kuimarisha vyama vya ushirika nchini, tume hiyo imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa Vyama vya Ushirika ili kuzalisha kwa tija na kuongeza uzalishaji kutokana na matumizi ya zana bora za kilimo. Amesema vyama vya ushirika 33 vimekopeshwa trekta moja kwa kila chama kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tume na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Bodi ya Pamba (TCB).
Pia, Waziri Mkuu amesema katika kuendeleza azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda, Vyama vya Ushirika vimeendelea kuwekeza katika miradi mingine ya kimaendeleo ambayo inaisaidia katika kuleta maendeleo.
"Hadi kufikia Juni 30, 2019 jumla ya Vyama vya Ushirika 104 vinamiliki viwanda vidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao wanayoyazalisha hali ambayo imeleta tija kwa jamii inayozunguka maeneo hayo”.
Amesema hadi Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 1.3 imetolewa kwa wanachama ikilinganishwa na sh. bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba 2017. Akiba na amana za wanachama katika SACCOS zimefikia sh. bilioni 575 na hisa sh. bilioni 79.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Punguza kilo tano kwa siku saba
NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...
-
Kiwanja kinauzwa kipo Dodoma Mahungu njia ya kwenda Singida kabala hujafika NALA. Kiwanja ni cha Makazi kinaukubwa wa Sqm 450 ( 15 X...
-
Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania...

No comments:
Post a Comment