Search This Blog
Saturday, July 20, 2019
Waziri Mkuu awafunda Watumishi wa Umma 'Serikali inapima matokeo'
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wawe na mipango ya kazi ambayo itaweza kupimika na kutoa matokeo.
“Kila mtumishi anapaswa awe na mpango kazi katika sekta yake na ni lazima aende kupima matokeo. Awamu hii, tunataka kuona matokeo ya kazi zenu.”
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Same kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, mjini Same.
“Watumishi mmeletwa kwenye wilaya hii ili muwahudumie wananchi. Tulioajiriwa, kazi yetu kubwa ni kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote uwe ni wa kabila, itikadi au rangi.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kwamba baada ya mchujo wa watumishi hewa, waliobakia wanapaswa kufanya kazi kwa bidii.
“Fanyeni kazi kwa bidii, msimamo wa Serikali hii ni kwamba hatumvumilii mtumishi ambaye si mwajibikaji, ni mwizi, mzembe au anaomba rushwa. Serikali hii hatuna muda wa kujadili matatizo ya watumishi, tunamalizana hapo hapo,” amesema.
Amewataka watumishi hao wasimamie utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo chama tawala.
“Mtumishi angalia sekta yako inasema nini, ifanyie kazi. Kama ni maji, tafuta ni wapi yanapatikana, changanua zinahitajika shilingi ngapi, tafuta njia ya kupata hizo fedha ili wananchi wapate maji.”
Kuhusu tabia ya kukaa ofisini, Waziri Mkuu amekemea tabia hiyo na kuwataka watumishi wote nchini waache tabia ya kukaa ofisini na badala yake waende vijijini kuwasikiliza wananchi.
“Watumishi wa umma msikae ofisini. Nendeni vijijini walau kwa siku nne za juma. Hizo mbili zinazobakia, zitumieni kuandaa taarifa. Nendeni huko ili wananchi wasipate usumbufu wa kuja hapa mjini kuwatafuta,” amesisitiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Punguza kilo tano kwa siku saba
NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...
-
Kiwanja kinauzwa kipo Dodoma Mahungu njia ya kwenda Singida kabala hujafika NALA. Kiwanja ni cha Makazi kinaukubwa wa Sqm 450 ( 15 X...
-
Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania...

No comments:
Post a Comment