Search This Blog

Wednesday, May 29, 2019

Serikali ya Poland yaonyesha nia ya kuisaidia Sekta ya Afya Nchini


Na. Enock Magali, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,  Selemani Jafo ameishukuru Serikali ya Poland kwa kuonyesha nia ya dhati ya kuisadia Tanzania katika Sekta ya Afya Nchini ili kuboresha na kupunguza changamoto katika Sekta hiyo.


Jafo ameyasema hayo wakati wa kikao na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya kutoka Poland cha kujadili masuala mbalimbali yanayouhusiana na Afya na jinsi Nchi hiyo inavyoweza kusaidia kuimarisha na kuboresha Sekta ya Afya nchini.

Jafo ameishukuru Serikali ya Poland  kwa ushirikiano wanatoa  katika Miradi mbalimbali ya maendeleo  na kutambua  umuhimu wa sekta ya afya nchini  kwa kuwa bila kuimarisha Sekta ya afya hakutakuwa na maendeleo na kushindwa kufikia uchumi wa kati.

“Sekta ya afya ni muhimu kwa jamii, jamii isipokuwa na afya bora hakutakuwa na maendeleo, hivyo ni vyema Serikali ikajikita kuwekeza katika Sekta ya afya kwa kuhakikisha inajenga miundombinu bora, uwepo wa vifaa na vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya nchini” Amesema Jafo.

Amesema kuwa  hatuwezi kufikia uchumi wa kati endapo watu  wetu hawatakuwa na afya bora, ili watu wafanyekazi kwa bidi waweze kuzalisha na kulipa kodi inavyotakiwa wanatakiwa kuwa na afya bora hivyo tunawakaribisha wadau mbalimbali wa Sekta ya afya kuwekeza katika Sekta hiyo.

Mhe. Jafo amendelea kuishukuru Serikali ya Poland kwa kuonyesha nia ya kuisaidia Serikali mkopo wenye gharama nafuu utakaosaidia kuimarisha na kuboresha sekta ya Afya nchini lengo likiwa ni kupunguza changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.

Ameiomba Serikali ya Poland kujikita zaidi katika kusaidia kwenye kuimarisha huduma za msingi hasa ujenzi wa Vituo vya afya na upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba  kwa kuwa ndipo kwenye changamoto kubwa  katika suala zima la utoaji wa huduma na itasaidia kupunguza vifo kwa jamii.

 Jafo amefafanua kuwa katika eneo la Sekta ya Afya Serikali itapata fursa ya kusaidiwa ujenzi wa Vituo vya afya, ambavyo vitakuwa vya mfano kwa kuwa na vifaa vyake  na kuwa na nyumba zaidi ya nne za madaktari  na hivyo kupunguza changamoto zilizopo.

Jafo amelishukuru shirika la Light For Africa kwa kuunganisha nchi ya Poland na Tanzania   ambao wameonyesha nia ya dhati katika kusaidia masuala ya Sekta ya Afya nchini jambo ambalo litasaidia kuleta maendeleo kwa jamii.

Aidha Wadau hao  watatembelea, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hospitali ya Mirembe, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma,  Hospitali ya Amana  na Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuangalia ni namna Tanzania inavyotoa huduma  za  afya na kuangalia maeneo ambayo wanaweza kusaidia katika kutumia fursa walizonazo.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...