Na, Baraka Messa, Songwe.
UGONJWA wa kuhara unaosababishwa na ulaji wa kinyesi kibichi umetajwa kuwa ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa vifo vya watoto wadogo walio chini ya miaka mitano.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omari Mgumba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi mazingira na matumizi bora ya vyoo,uliofanyika kimkoa katika viwanja vya kituo cha malori, Mjini Vwawa, Wilayani Mbozi.
Alisema Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ugonjwa unaoongoza kwa vifo vya watoto wadogo chini ya miaka mitano ni Nimonia, lakini ugonjwa unaofuatia ni kuhara, kunako sababishwa na kula kinyesi kibichi hususani wakati wa unyonyeshaji kwa akina mama .
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika linalohudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) inaonyesha kuwa magonjwa ya homa ya mapafu (Nimonia) na ule wa kuhara huua watoto milioni mbili kila mwaka sawa na asilimia 29 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani kote.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa aliitaka jamii hususani akina mama kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafi kwa kunawa mikono kabla ya kuanza kunyonyesha watoto wao
Akizungumzia kuhusu matumizi bora ya vyoo, Mgumba alisema hadi kufikia sasa mkoa huo umetekeleza zoezi hilo la matumizi ya vyoo bora kwa asilimia 63 tuu.
"Takwimu zinaonyesha katika mkoa wetu wa Songwe zoezi la kampeni ya vyoo bora tumefikia asilimia 63 hii sawa na kwamba, kwenye kila kaya 100, kaya 60 ndio zina vyoo bora".
Aliongeza kuwa, hadi kufikia mwaka 2023 kila kaya katika mkoa huo itakuwa na choo bora hivyo utekelezaji wa kampeni hiyo kufikia asilimia 100.
No comments:
Post a Comment