Shirika la Ndege la Uswisi (EDELWEISS) imezindua safari zake za moja kwa moja kutoka Uswisi kuja Tanzania.
Ndege hiyo aina ya Airbus A343 imetua nchini leo Jumamosi ya Oktoba 9, 2021 kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikiwa na abiria 270.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chasot walikuwa uwanjani hapo kuipokea ndege hiyo ambayo abiria 160 wameshuka KIA na wengine 110 wanakwenda visiwani Zanzibar.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO), Christine Mwakatobe, amesema ujio wa ndege hiyo ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza na kuvutia zaidi watalii.
Amesema miongoni mwa faida ni kuongeza makusanyo ya KIA pamoja yale ya wadau wengine kama wa utalii na sekta ya anga nchini.
Kwa upande wake, Profesa Mbarawa amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, lakini janga la ugonjwa wa Uviko-19 liliathiri kasi ya watalii kuja nchini.
"Serikali imejipanga kuhakikisha miundobinu ya barabara na viwanja vya ndege inaboreshwa ili kuvutia watalii, na mataifa makubwa duniani ya ndege yaone umuhimu wa kuanzisha safari kuja nchini," amesema.
Naye Dk Ndumbaro amesema ujio wa ndege hiyo ni juhudi za Serikali kufufua utalii na ni kiashiria kwamba, Tanzania iko salama katika janga la Uviko-19.
No comments:
Post a Comment