Juma Simba (45) mkazi wa kijiji cha Kitembere wilayani hapa mkoani Mara, jana Oktoba 5 alihukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kukiri kukamatwa na ngozi kavu ya fisi na miguu miwili ya nyuma ya nyumbu.
Simba aliyeonekana mtulivu kipindi chote alipokuwa mahakamani hapo alikiri makosa yote matatu ya uhujumu uchumi aliyosomewa mahakamani hapo.
Mwendesha mashitaka wa Jamhuri, Meikasi David akisoma hati ya Mashitaka katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 49/2021 mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya Adelina Mzalifu, amesema mshitakiwa anakabiliwa na makosa matatu.
Kosa la kwanza ni kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti bila kibali, kosa la pili kukutwa na silaha aina ya panga ndani ya hifadhi bila kibali na la tatu ni kukutwa na ngozi kavu ya fisi yenye thamani ya zaidi ya Sh1.26 milioni na kukutwa na miguu miwili ya nyuma ya nyumbu mwenye thamani ya zaidi ya Sh1.49 milioni mali ya serikali kinyume cha sheria.
Kukiri kwake kuliifanya mahakama kutulia kidogo wakati hakimu akiandika kisha akasema, kutokana na makosa aliyotenda na kukiri mbele ya mahakama kuwa adhabu ni miaka 30 gerezani na kuwa milango ya rufaa iko wazi.
No comments:
Post a Comment