Search This Blog

Sunday, October 17, 2021

Halmashauri ya jiji la Mwanza lawa mfano bora kwa anuani za makazi


Na Maridhia Ngemela, Mwanza.

 Kila nyumba itakuwa na namba yake ili kutambulika kirahisi na mitaa kuwa na majina ikiwa ni njia moja wapo ya kupata msaada kwa haraka.

Serikali imetenga shilingi bilioni 45 za kutekeleza mpango wa anuani za makazi na postikodi nchini kwa kujenga miundombinu ya anuani hizo kwenye halamshauri 194 nchi nzima zilizopo Tanzania Bara na Visiwani zoezi hilo lilianza mwaka 2019. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji wakati akiwa ziarani mkoani Mwanza kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo kwenye Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwa ni eneo la mfano ili kujifunza kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa zoezi hilo  ili kuzifikia halmashauri zote 194 nchini ambapo halmashauri 184 ni za Tanzania Bara na halmashauri kumi ni za Zanzibar 

“ Jiji la Mwanza kulikuwa ni mfano kwahiyo lengo ni  kujifunza na kuhakikisha kuwa kila mtaa unakuwa na jina lake na kila nyumba iwe na namba yake, hii inarahisisha utendaji kazi wa Serikali hata ndani ya jamii kwenye shughuli zetu za kiuchumi, tunaongelea kuwa na uchumi wa kidijitali, uchumi wa kidijitali hauwezekani bila kuwa tumekamilisha mfumo huu wa anuani za makazi, tunamshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia shilingi bilioni 45 ndani ya Wizara yangu kwa zoezi hili tu kwahiyo tunakwenda kukamilisha kwenye mitaa yetu . ” amesema Dk Kijaji 

Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuwafikia wananchi kule walipo ili mwananchi anapopata tatizo, iwe ameunguliwa na moto pale alipo ni rahisi kuwapigia zimamoto na kuwaarifu mtaa na nyumba ulipo, au una mgonjwa unahitaji huduma ya gari ya wagonjwa, unaawarifu wanakufikia na kwa mwananchi aliyeagiza mzigo au kifurushi kutoka nje ya nchi hana sababu ya kwenda posta kufuata mzigo bali mzigo wako utaletwa mpaka ulipo ili wananchi watumie muda wao mwingi kujiletea maendeleo yao

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kazi hii ya utekelezaji wa anuani za makazi nchi nzima utatekelezwa na wananchi wenyewe waliopo kwenye maeneo hayo na itatoa ajira kwa wananchi hao na ametoa rai kwa wananchi kuwa tayari kujitokeza kutekeleza mpango huo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa wananchi wana kiu ya kujulikana kwa kuwa sasa mitaa yao ina majina na nyumba zao zina namba ambapo mwananchi analetewa mzigo wake pale alipo kwa kuwa sasa anatambulika mahali anapoishi.


Diwani wa Nyamagana, Bhiku Kotecha akizungumza kwa niaba ya wananchi wake ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mpango wa zoezi hilo la kuweka namba za makazi kwa kuwa mradi huu una tija kwa wananchi, wananchi wake wamefurahi kwa kuwa mwananchi akipata ajali anaeleza moja kwa moja mahali alipo na anapata huduma kwa haraka. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam wa Anuani za Makazi na Postikodi, Hlamashauri ya Jiji la Mwanza ndugu Moses Seleki amesema kuwa jumla ya nyumba 108,000 zimefungwa namba za nyumba, nguzo 5,800 zimewekwa zenye vibao vya majina ya mitaa na nyumba 98,000 zimeingizwa kwenye mfumo wa anuani za makazi kwa simu ya mkononi.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...