Search This Blog

Thursday, September 30, 2021

Mwigulu Aagiza Halmashauri Nne Zichunguzwe


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), azikague na kuzichunguza halmashauri nne za wilaya na taasisi ya serikali kwa tuhuma za kukiuka Sheria za Ununuzi wa Umma.


Dk Mwigulu alitoa agizo hilo jijini Dodoma baada ya kupokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ya Mwaka wa Fedha 2020/2021.


Alisema lazima ufanyike uchunguzi hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika kukiuka taratibu za ununuzi ikiwa ni pamoja na kutoa zabuni nje ya mfumo wa kielektroniki wa TANePS unaotumika kuchakata zabuni.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi (PPRA), Profesa Ninatubu Lema kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA,  Profesa Marten Lumbanga, taasisi tano zilipata wastani hafifu wa kufuata sheria taratibu na kanuni za ununuzi wa umma.


Nazo ni Halmashauri ya Mji Kondoa, Halmashauri ya Mbogwe, Halmashauri ya Biharamulo, Halmashauri ya Chato na Taasisi ya Utafiti wa Wanyama.


Dk Mwigulu pia alimuagiza Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, aziandikie waraka taasisi 172 zilizounganishwa TANePS zijieleze kwa nini hazitumii mfumo huo kufanya ununuzi.


Alizitaka taasisi nunuzi zote zitumie asilimia 30 ya gharama zao za zabuni zinazotangazwa katika mpango wa ununuzi wa mwaka kwa ajili ya kuwezesha makundi maalumu yakiwemo ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.


"Nimesikitika sana baada ya kusikia kwamba kati ya taasisi 86 mlizozikagua ni taasisi mbili tu ndizo zilitenga asilimia 30 katika mpango wao wa ununuzi wa mwaka kwa ajili ya makundi maalumu," alisema Dk Mwigulu.


Tutuba alisema atazingatia maelekezo aliyopewa na kuwawajibisha wote watakaobainika kuhusika na ukiukaji wa sheria ya ununuzi.


Alizitaka taasisi za umma zizingatie sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma ili kuthaminisha miradi ya maendeleo na fedha zinazotumika.


Kwa mujibu wa Tutuba, katika mwaka wa fedha 2020/2021 bajeti ya ununuzi ilikuwa shilingi trilioni 25 sawa na zaidi ya asilimia 75 ya bajeti yote ya serikali.


Profesa Lema alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021 walifanya ukaguzi wa mikataba 8,838 ya ununuzi yenye thamani ya Sh trilioni 9.2 kutoka taasisi 86.


 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...