Mama yake Waziri mkuu wa Uingereza Charlotte Johnson Wahl amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79.
Taarifa iliyochapishwa katika gazeti la Times nchini Uingereza inasema amefariki kifo cha "ghafla na cha amani" katika hospitali ya St Mary magharibi mwa London.
Boris Johnson wakati mmoja alimuelezea mama yake, ambaye alikuwa mchoraji kama mwenye "mamlaka ya juu zaidi " katika familia.
Watu maarufu kutoka vyama vyote vya kisiasa, akiwemo kiongozi wa chama cha Labour Sir Keir Starmer, wametuma salamu za rambirambi kwa Bw Johnson.
Katika ujumbe wake wa Twitter Sir Keir aliandika : "Pole sana, nimepata taarifa ya waziri mkuu kumpoteza mama yake. Natoa rambirambi kwake binafsi na kwa familia yake."
Bi Johnson Wahl, ambaye baba yake alikuwa rais wa Tume ya Ulaya ya haki za binadamu katika miaka ya 1970, aliolewa na Stanley Johnson mwaka 1963 kabla ya kumaliza shahada yake katika Chuo kikuu cha Oxford kama mhitimu wa kwanza wa kike kumaliza masomo ya shahada chuoni hapo akiwa ameolewa.
Wawili hao walikuwa na watoto wanne - Boris, mwandishi wa habari Rachel, waziri wa zamani wa mazingira Jo na mwanamazingira Leo. Ndoa yao ilivunjika 1979.
Kama msanii wa uchoraji, Bi Johnson Wahl alitengeneza jina lake kama mchoraji wa picha, ambapo wasanii wa maigizo Joanna Lumley na author Jilly Cooper wakiwa miongoni mwa watu aliowachora.
Mnamo mwaka 1988, aliolewa na Profesa Mmarekani Nicholas Wahl na akahamia New York – ambapo alianza kuchora michoro ya jiji. Alirejea London baada ya kifo cha mume wake mwaka 1996.
Akiwa na umri wa miaka 40, alipatwa na maradhi ya ubongo ya Parkinson, lakini aliendelea kuchora, akitembea kwa usaidizi wa kifaa cha kutembea.

No comments:
Post a Comment