Na Amiri Kilagalila,Njombe.
Madiwani wa halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe wamelalamikia kitendo cha wataalam wa halmashauri kutekeleza baadhi ya miradi ya kimaendeleo bila kushirikishwa ikiwemo mradi wa ujenzi wa ukumbi pamoja na matumizi ya fedha zaidi ya milioni mia saba.
Wakizungumza katika kikao cha baraza la madiwani ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo wamesema kuwa wanashangazwa na wataalam hao kwa kuwa kuna fedha zaidi ya milioni mia saba ambazo zilitolewa kwaajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi za halmashauri hiyo hawajui zimetumikaje na wanashangaa kuona ukumbi unajengwa bila wao kupewa taarifa.
“Fedha zimeletwa kwa faida ya wananchi na sisi ndio tunasimamia wananchi tunawaambia simama hapa pana mashaka wewe unasema unaendelea unamtumikia nani?”alisema mmoja wa madiwani kwenye baraza
“Kusimamisha lile jengo kwa kuwa lilienda tofauti ilikuwa ni busara sana nikupe pole sana mwenyekiti na kamati yako baada ya kutoa kauli yako ilipuuzwa na shughuli zikaendelea na ninapata mashaka hata katika baraza hili tunaweza tukatoa kauli watu wakapuuza”aliongeza diwani mwingine
Kutokana na kukosekana kwa ushirikishwaji katika ujenzi wa ukumbi huo,baadhi ya madiwani ambao ni wajumbe wa kamati ya fedha akiwemo Diwani wa kata ya mahongole MARIO KIHOMBO na diwani wa kata ya mjimwema NOLASKO MLOWE,wamesema wamelazimika kuzuia ujenzi wa ukumbi huo mpaka pale watakapopewa taarifa za ujenzi wa mradi huo.
“Zipo shughuli ambazo watendaji wetu wameendelea kuzifanya kwa bahati mbaya hatukuweza kupata taarifa lazima tufike mahali tusitishe baadhi ya shughuli ambazo inafika mahali wenzetu wanafanya bila taarifa kwa hiyo zipo kazi nyingi zimefanyika bila taarifa na madhara yametokea”alisema Mario Kihombo
Naye Nolasko Mlowe alisema “Toka tumeingia tulianza kudai taarifa ya jengo hili taarifa haziji na kazi zilizidi kuendelea”
Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Makambako Hanana Mfikwa amesema kuwa amedai taarifa za utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa ukumbi pamoja na matumizi ya fedha hizo zaidi ya milioni mia saba kwa zaidi ya miezi sita lakini hajapewa mpaka hivi sasa.
“Na mpaka sasa sijapata taarifa sijui feniture inachongwa wapi,iliingia shilingi ngapi ni furniture ya aina gani sina taarifa hiyo.Tumekwenda miezi sita taarifa hii haijapatikana”alisema Mfikwa
Hata hivyo kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa makambako Appia Mayemba amewaomba radhi madiwani kwa kosa la kutoshirikishwa na kufafanua kuwa ndani ya mwezi mmoja watapewa taarifa juu ya matumizi ya fedha hizo na ujenzi wa ukumbi huo.
“Mh, mwenyekiti kwanza kwa heshima kubwa tunaomba mtuwie radhi kwa yale yaliyojitokeza na ni changamoto ambazo zinaweza kujitokeza katika shughuli zetu ninaomba jambo hili lirudi kwenye kamati ya fedha kwa ajili ya mchakato na baadaye tutaleta majibu sahihi kadiri ya wajumbe walivyokuwa wanahoji”alisema Appia Mayemba
No comments:
Post a Comment