Nchini Ufaransa takribani mikusanyiko 200 ya kupinga masharti ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona imefanyika jana Jumamosi.
Huu ni muendelezo wa mingine kadhaa iliyofanyika kwa majuma manane yaliopita katika maeneo tofauti ya taifa hilo.
Kama ilivyokuwa kwa maandamano mengine yaliyopita haya pia yalizingatia katika kupinga pasipoti ya afya kama inavyohitajiwa na Rais wa taifa hilo Emmanuel Macron kwa lengo la kuboresha hatua ya utoaji chanjo, uhitaji wa cheti kinachoonesha huna maambukizi pamoja na ulazima wa kuchanja kwa makundi kadhaa ya kitaalumu wakiwemo wa sekta ya afya.
Kwa mujibu wa mamlaka za miji, takribani watu 6, 000 waliingia mitaani katika mji wa kusini mwa Ufaransa wa Montpellier, wengine 4,000 mji wa Avignon na wengine zaidi ya 18,000 mjini Paris.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imesema jumla ya watu 140,000 wameandamana katika maeneo yote hayo tofauti nchini kote.

No comments:
Post a Comment