Kundi la Taliban nchini Afghanistan limeongeza idadi ya viongozi katika baraza lake la mawaziri la mpito kwa kuongeza mawaziri kadhaa na manaibu wao ingawa limeshindwa kumteua mwanammke hata mmoja kuingia kwenye baraza hilo.
Hatua hiyo imeonesha namna kundi hilo lilivyoshikilia mwelekeo wake wa msimamo mkali licha ya kutolewa miito na jumuiya ya kimataifa ya kuukemea mwelekeo huo baada ya mpangilio wa mwanzo wa baraza lake la mawaziri kujumuisha wanaume watupu mwanzoni mwa mwezi huu.
Jumuiya ya Kimataifa imesema italihukumu kundi la Taliban kwa kutazama vitendo vyake na hatua ya kuitambua serikali wanayoiongoza itatokana na namna wanawake na makundi ya wachache wanavyoangaliwa.
Msemaji wa serikali ya Taliban, Zabihullah Mujahid akizungumza na wandishi habari leo amesema kuna uwezekano wa kujumuishwa wanawake kwenye baraza hilo wakati mwingine lakini hakutoa maelezo zaidi.
Mujahid ametetea hatua hiyo ya kuongezwa idadi ya watu katika baraza hilo akisema wameongeza wanachama wa jamii za makabila ya wachache kama vile jamii ya Hazara.

No comments:
Post a Comment