Search This Blog

Wednesday, September 29, 2021

Kama si makubaliano ya Doha, Afghanistan isingeangukia mikononi mwa Taliban- Maafisa wa ulinzi


Maofisa wa ngazi za juu wa Ulinzi wa Marekani wamesema hatua ya Taliban kurejea madarakani nchini Afghanistan ilitokana na mkataba kati ya kundi hilo na utawala wa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump.

Mkataba huo uliojulikana kama makubaliano ya Doha ulisainiwa Februari 2020 na kuweka tarehe ya kuondoka kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani kwenye ardhi ya Afghanistan.

Jenerali Frank McKenzie alisema makubaliano hayo yalikuwa "na athari mbaya" kwa serikali ya Afghanistan na Jeshi lake.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Waziri wa ulinzi Lloyd Austin anayesema makubaliano hayo yaliisaidia kikundi cha Taliban kujiimarisha zaidi.

Mbali na kuweka tarehe ya mwisho ya vikosi vya Marekani kuondoka Afghanistan, makubaliano ya Doha yalijumuisha pia majukumu mapana kwa Taliban kuchukua hatua za kuzuia makundi kama vile al-Qaeda kutishia usalama wa Marekani na washirika wake.

Baada ya kuchaguliwa kwake, Rais wa Marekani Joe Biden aliendeleza mpango huo wa Marekani kujiondoa lakini kwa kuongeza muda mpaka Agosti 31, badala ya mwezi Mei.

Maafisa hao wa ulinzi wa Marekani wameyasema hayo Jumatano hii mbele ya Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo.

Kikao hicho kinafanyika wiki kadhaa baada ya vurugu zilizotokea katika uwanja wa ndege wa Kabul wakati mataifa ya kigeni yakijaribu kuwarejesha raia wao nyumbani huku maelfu ya raia wa Afghanistan waliokata tamaa wakijaribu kuikimbia nchi hiyo. Wakati wa heka heka hizo shambulio la kujitoa mhanga kwenye uwanja huo liliuwa watu 182.

Jenerali McKenzie alisimamia zoezi la kuondoka kwa vikosi vya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, lililohitimisha miaka 20 ya uwepo wake nchini humo ikiwa ni vita vya muda mrefu zaidi katika historia ya Marekani.

Jenerali McKenzie aliiambia kamati hiyo kwamba makubaliano ya Doha yalikuwa na athari kubwa ya kisaikolojia kwa serikali ya Afghanistan kwa sababu iliweka tarehe ya "lini watarajie misaada yote ya kijeshi kukoma".

Alisema alikuwa akiamini "kwa muda mrefu" kwamba kama Marekani itapunguza idadi ya wanajeshi ama washauri wake wa kijeshi nchini Afghanistan na kuwa chini ya 2,500, serikali ya Afghanistan na jeshi lake lingeanguka bila shaka.

Baada ya makubaliano ya Doha, alisema agizo la kupunguzwa kwa wanajeshi lililotolewa na Rais Biden mwezi Aprili lilikuwa "msumari mwingine katika jeneza".

Austin alisema ahadi ya Marekani ya kusitisha mashambulizi ya anga dhidi ya Taliban, makubaliano ya Doha yalimaanisha kuwa kundi hilo la Kiislamu "lilipata nguvu zaidi, waliongeza operesheni zao za mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama vya Afghanistan, na Waafghanistan wengi waliuawa kila wiki".

Maafisa hao wa ulinzi Jumanne wiki hii walihojiwa pia na Kamati ya Huduma za Kijeshi ya bunge la Seneti, ambapo Jenerali Milley na Jenerali McKenzie walisema walipendekeza kusalia kwa wanajeshi 2,500 nchini Afghanistan, kabla ya zoezi la kujiondoa kabisa mwezi Agosti.

Jenerali Milley pia alisema kuwa hatua ya Taliban kuidhibiti upya Aghanistan itafanya zoezi la kwalinda Wamarekani dhidi ya mashambulizi ya kigaidi kuwa gumu, huku akilielezea kundi hilo kama kundi la kigaidi na ambalo "bado halijavunja uhusiano wake na al-Qaeda".

Akizungumza na BBC siku ya Jumatano, msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid alisema wanamgambo hao "wameuhakikishia ulimwengu kwamba hakutakuwa na tishio lolote dhidi ya nchi yoyote utakaofanywa kutoka kwenye ardhi ya Afghanistan ikiwemo Marekani".

"Tumejitolea kutekeleza makubaliano yaliyotiwa saini mjini Doha kati ya Afghanistan na Marekani. Tunataka pia Wamarekani na washirika wake na wao wajitolee kulinda makubaliano hayo. Badala ya kutoa maoni hasi itakuwa bora kwao kuchagua njia ya diplomasia na ushirikiano," alisema.

 




No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...