Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka la kutaka vyombo vinavyotoa usafiri wa umma, hususan daladala kutosimamisha abiria, limewaibua wamiliki wa vyombo hivyo wakilalamikia hasara iwapo agizo hilo litatekelezwa.
Uongozi wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (TDA), umesema kuwa wanapata hasara kwa kutosimamisha abiria kwa kuwa bei ya mafuta imezidi kupanda.
Malalamiko hayo yamekuja wakati Mtaka akitoa agizo hilo, ikiwa ni mkakati wa kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona, ambapo ameagiza mabasi ya abiria yanayofanya safari zake ndani ya mkoa huo, daladala, bajaji na bodaboda kubeba abiria kulingana na uwezo wa chombo husika.
Mtaka alitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Covid-19 mkoani hapa, huku akionya kwamba, hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokwenda kinyume.
Hata hivyo, tangu kutolewa kwa agizo hilo ni kama utekelezaji wake umekwama, kwani daladala zimeendelea kusimamisha abiria, bajaji zinajaza na bodaboda zimeendelea kubeba mshikaki kama kawaida.

No comments:
Post a Comment