Search This Blog

Tuesday, August 10, 2021

Waasi wa Tigray wakana kuhusika na shambulio baya dhidi ya hospitali jimbo la Afar


Waasi wa Tigray wamekanusha kuhusika na shambulio kwenye kituo cha afya katika jimbo la Afar huko Ethiopia, ambalo liliwauwa watu wasiopungua 12.

Utawala wa mkoa wa Afar unalaumu vikosi vya Tigray kwa shambulio hilo, wakati mapigano katika mzozo wa miezi tisa wa Ethiopia ukizidi hadi katika majimbo yanayopakana na Tigray.

Daktari katika mkoa wa Afar wa Ethiopia aliambia BBC kwamba watu hao 12 walifariki kutokana na majeraha waliyoyapata katika shambulio kali la silaha katika kituo cha afya cha Galikoma.

Watu zaidi ya 30 wakiwemo wanaume ,wanawake na watoto walihitaji matibabu ya dharura baada ya shambulio hilo .

Msemaji wa utawala wa jimbo la Afar alisema raia wengi zaidi walifariki katika eneo la tukio lakini hakuweza kutoa idadi rasmi ya vifo.

Alilaumu vikosi vya Tigray - lakini msemaji wa Tigray People's Liberation Front alisema kwenye Twitter kwamba ripoti za shambulio hilo "ni za kutisha".

Alikana kuhusika kwa kundi hilo na kusema wako tayari kushirikiana na uchunguzi wowote kubaini ukweli

Kituo hicho cha afya kilitumika kuwahifadhi watu waliokimbia makazi yao na kuweka msaada wa chakula.

Wiki iliyopita mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alizuru Ethiopia na kusema idadi ya wakaazi wa Afar walioachwa bila makao kwa sababu ya mapigano ya hivi karibuni ni 54,000.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...