MBUNGE wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulipatia jimbo lake kiasi cha Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya kutatua changamoto ya barabara za vijijini zilizopo ndani ya Jimbo lake.
Kunambi ametoa shukrani hizo katika Kijiji cha Tanganyika kilichopo Kata ya Masagati ambapo alifika kukagua miundombinu na miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa kwenye kata hiyo.
Amesema Serikali imewapatia Wabunge wote kiasi cha Sh Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za mitaa na vijiji lakini yeye amepata nyongeza ya Sh Bilioni Moja na hivyo kutoa shukrani zake kwa Rais Samia.
"Mbunge wenu tayari Nimepokea kiasi cha Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya barabara zetu za ndani, nnavyozungumza na Nyinyi wenzetu wa TARURA wanaendelea na usanifu wa barabara hizi ili kusudi watagaze tenda wakandarasi waanze kazi, naamini Oktoba mwaka huu Mkandarasi atakua kazini.
Kuhusu kupata daraja la kudumu la Mto Mfuji hapa Masagati, Serikali imeshanipa fursa ya kutoa mapendekezo ya kujengewa madaraja matatu jimboni kwangu, nimeshapendeza Daraja la Mto Mfuji hapa, Mngeta na Chiwachiwa, kwahiyo yote yatafanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu ili ujenzi wake uanze,"Amesema Kunambi.
Akizungumzia ujenzi wa Zahanati ya Tanganyika ambayo inajengwa kwa ushirikiano wa Wananchi, Ofisi ya Mbunge na Serikali amesema tayari imefikia kiwango kizuri huku akihamasisha wananchi hao kuungana tena pamoja kujenga nyumba za madaktari watakaokua wakiwahudumia.
"Mbunge wenu nimepambana tumepata Daktari hapa Tanganyika kati ya wahudumu wa Afya 37 walioletwa jimboni kwetu na sisi Tanganyika tumepata mmoja, hivyo ni vema tushirikiane tena kwa pamoja kujenga nyumba ya wahudumu hawa ili wasikae umbali mrefu na Zahanati yetu, kufanikisha hili kutatusaidia kupata huduma muda wowote maana kuna uhakika wa Daktari kuwepo karibu," Amesema Kunambi.
Kuhusu umeme kwenye kijiji hiko, Kunambi amewaahidi wananchi hao kuwa hadi kufikia Aprili, 2022 umeme utakua unawaka Tanganyika kwani kupitia Mpango wa REA tayari tathmini ishafanyika na kilichobakia ni umeme kuletwa na hivyo kuwahakikishia kuwa umeme utawaka.


No comments:
Post a Comment