Rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano ametoa wito kwa serikali kutathmini uwezekano wa kujadiliana na makundi yenye silaha yanayohudumu katika eneo la Cabo Delgado linalokumbwa na mzozo.
Anasema kuna “aina flani ya ugaidi” ambao umekomeshwa kupitia majadiliano.
“Huenda pengine kiongozi wa kundi hilo naonesha ishara ya kutaka kutupatia nafasi ya majadiliano ambayo yatasaidia kumaliza” ghasia za silaha,alikiambia kituo cha Radio Mozambique kinachomilikiwa na serikali, katika mahojiano siku ya Jumatano.
Rais huyo wa zamani wa Msumbiji alisema sababu za vurugu za silaha huko Cabo Delgado lazima zichunguzwe kama njia ya kutatua mzozo wa kijeshi na kijamii katika jimbo hilo.
Bwana Chissano alikuwa rais wa Msumbiji kati ya 1986 na 2005. Aliongoza mazungumzo ya mafanikio na waasi wa zamani wa upinzani wa Msumbiji (Renamo), ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 16 mwaka 1992.
Rais wa sasa, Filipe Nyusi, ameelezea nia yake ya kujadiliana na vikundi vyenye silaha lakini amelalamika kuwa waasi hawajaonesha "ishara" ya kukaribisha mazungumzo hayo.
Mkoa wa Cabo Delgado umetumbia kwenye ghasia tangu mwaka 2017, baadhi ya mashambulio yakidaiwa kufanywa na kundi la Islamic State.
Mashambulio hayo kufikia sasa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000 na wengine zaidi ya 800,000 kufurushwa makwao.

No comments:
Post a Comment