Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amehimiza kusitishwa mara moja kwa mapigano ya ndani kati ya makundi mawili ya kijeshi ya vuguvugu la hasimu wake wa zamani ambaye ni Makamu wa Rais Riek Machar baada ya machafuko ya mwishoni mwa wiki kusababisha vifo vya zaidi ya watu 30.
Wito wa Kiir umekuja wakati Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Mashariki mwa Afrika - IGAD ikionya kuwa kuvunjika kwa vuguvugu la Machar la Sudan People's Liberation Movement/Army-In Opposition - SPLA-IO ni zaidi ya mgogoro wa ndani ya chama na unaweza kusababisha athari kubwa za sasa na siku za usoni kwa taifa hilo changa ulimwenguni.
Kufuatia mkutano jana na Machar na mawaziri wenngine wa serikali, ofisi ya Kiir ilitoa taarifa ikitaka kusitishwa kwa uhasama kati ya kambi hizo mbili. Mkutano wa dharura wa Jumatatu wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa IGAD ulizitaka pande zinazohasimiana kuanzisha mazungumzo.

No comments:
Post a Comment