Search This Blog

Friday, August 6, 2021

Naibu Waziri Ndejembi ahimiza ushirikiano wa pamoja kwa Taasisi za Umma katika kutekeleza majukumu yao


NAIBU Waziri  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amezitaka Taasisi zote za Umma nchini kuwa na utamaduni wa  kushirikiana na kupeana mrejesho wa utendaji kazi ili kuepuka migogoro ya kiutendaji baina yao kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya utendaji kazi wa Taasisi za Serikali kwa Umma.

Ndejembi ametoa wito huo kwa Taasisi za Umma wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Umma mkoani Katavi kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani humo.

Ndejembi amesema, ni jambo la kushangaza pale kiongozi anapokwenda kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Serikali katika eneo lake la utawala na kubaini baadhi ya taasisi kutoshirikiana kiutendaji na badala yake zinatupiana lawama.

“Inakuaje Watumishi wanaohusika na masuala ya ardhi wanakwenda kubomoa nyumba inayodaiwa kujengwa kinyume na utaratibu, wakati nyumba hiyo imepewa huduma ya maji na umeme na Taasisi nyingine za Serikali," Ndejembi amehoji.

Ameongeza kuwa, mgogoro kama huo unatokana na baadhi ya Taasisi za Umma kutoshirikiana na kutopeana mrejesho kiutendaji.

Pia, Ndejembi amesisitiza kuwa Taasisi za Umma zinategemeana kiutendaji hivyo zinapaswa kujenga utamaduni wa kupeana mrejesho ili kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau.

Pamoja na kusisitiza taasisi za umma kushirikiana, Ndejembi amehimiza  ushirikiano wa kiutendaji ndani ya Taasisi za Umma  na kuhoji kwanini kuwe na kazi inafanywa na taasisi mojawapo ya Serikali ndani ya Sekretarieti ya Mkoa lakini Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) hajapewa taarifa, hivyo amezitaka taasisi za umma kuacha kufanya kazi kimazoea.

“Ni mara nyingi mambo yanaendelea ndani ya taasisi hususani yenye maslahi wakati viongozi wa juu wa taasisi hiyo hawana taarifa yoyote, lakini jambo likiharibika wao ndio wanawajibika kutoa taarifa Serikalini," Amesema Ndejembi.

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Catherine Mashalla amemshukuru Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji na kutoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa ni dira ya utendaji kazi unazingatia weledi kwa watumishi wote mkoani humo.

Mashalla amemuahidi Ndejembi kuwa, yeye na viongozi wenzie watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa ili wananchi wapate huduma bora.

Naibu Waziri Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Mkoani Katavi yenye lengo la kukutana na Watumishi wa Umma ili kusikiliza kero, changamoto zinazowakabili na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao mkoani humo.


No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...