Search This Blog

Saturday, August 28, 2021

Dk Rwiguza awahimiza wazazi kuzingatia watoto wanakunywa maziwa kila wakati


WAZAZI nchini wamehimizwa kuweka mkazo katika kuwapatia watoto wao lishe bora ikiwemo kuhakikisha wanakunywa maziwa kila wakati ili kuwafanya wawe na afya nzuri itakayowasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Asimwe Rwiguza wakati akizindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji Maziwa Shuleni uliyofanyika Mkoani Kilimanjaro Agosti 27, 2021.

Wakati akizindua kampeni hiyo Dkt. Rwiguza amesema kuwa jukumu la lishe lipo mikononi mwa wazazi hivyo ni muhimu wakajitahidi kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kugharamia lishe ya watoto  wao.

"Natoa wito kwa wazazi wote nchini kuona umuhimu wa kuwapa maziwa watoto,  faida za unywaji wa maziwa kwa watoto zinafahamika sitaki kuzirudia hapa, maziwa yatawajenga, watakuwa na akili na kuwasaidia kufanya vizuri katika masomo yao," Amesema Dk Rwiguza

Aliongeza kuwa uzinduzi huo wa awamu ya pili uwe chachu kwa jamii kuhakikisha watoto wao wanakunywa maziwa ya kutosha na zile changamoto zilizoonekana wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika awamu ya kwanza zishughulikiwe ili mafanikio yaweze kupatikana.

Naye,  Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk George Msalya amesema kuwa kufuatia uzinduzi wa kampeni hiyo ni muhimu sasa kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa maziwa ili kufanya maziwa hayo kupatikana kwa wingi na wakati wote hatua ambayo itawawezesha wawekezaji  kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

"Maziwa yanayoingia katika mfumo rasmi wa uchakataji katika Viwanda vyetu ni chini ya asilimia 3 ya maziwa yote yanayozalishwa hapa nchini, hiyo ni asilimia ndogo ukilinganisha na nchi za wenzetu, hivyo ni muhimu kuhamasisha wawekezaji ili kukuza tasnia hii ya maziwa nchini," Amesema Dk Msalya

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, kinachojishughulisha na uchakataji wa Maziwa Mkoani Kilimanjaro, Hellen Ussiri amesema kuwa baada ya Serikali kutoa tamko la uhamasishaji wa unywaji wa maziwa shule bado kumekuwa na mwamko mdogo hivyo Chama hicho kimefanya jitihada za kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni.

"Kiwanda cha Nronga kitasambaza maziwa kwa shule 10  za msingi zilizopo katika Wilaya ya Hai zenye jumla ya Wanafunzi 6151 ili kuendelea kutoa hamasa ya Unywaji wa maziwa kwa watoto," Amesema Ussiri.

Aidha, alitoa rai kwa wadau mbalimbali wa biashara  pamoja na wazazi kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizo ili walau adhma ya kuwapatia watoto wa shule maziwa mara mbili kwa wiki iweze kufanikiwa.


No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...