Search This Blog

Friday, August 6, 2021

DC akemea utoro wa wanafunzi shuleni siku za mnada


NA TEGEMEO KASTUS

Wazazi muache tabia ya kuwapeleka watoto mnadani na kuacha masomo shuleni, serikali inajenga miundo mbinu mizuri ili kuboesha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Watendaji wa elimu na viongozi wa Halmashauri za vijiji wanapaswa kusimamia ili kuondoa utoro wa wanafunzi siku za minada. Elimu ni chachu ya maendeleo kwa jamii, tunahitaji kuwapa maarifa ya kutosha vijana wetu ili tuweze kuinua kiwango cha ufaulu ili iweze kuwasaidia katika maisha yao baadae.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati wa uzinduzi wa madarasa mawili na matundu thelathini na mbili ya vyoo. Amehimiza wanafunzi kuzingatia masomo na kuwa na mahudhurio mazuri shuleni, amesema shule ya msingi Bonde la Faru imekuwa na ufaulu wa 100%. Amepongeza walimu na wanafunzi kwa ufaulu mzuri wa mtihani wa taifa mwaka jana na ameomba walimu kuendeleza rekodi nzuri ya ufaulu waliyonayo katika shule ya Msingi Bonde la Faru.

Mh. Kayanda amewapongeza wafadhili wa ECLAT Foundation (Tanzania) kwa kushirikiana na  Upendo society (Germany) kwa ujenzi huo wa vyumba viwili vya madarasa. Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo wa elimu, amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kufanya mambo makubwa katika elimu kwa sasa imetoa kiasi cha million 112 kwa ajili ya kukamilisha maboma 10 ya madarasa katika shule za msingi. Ameongeza kusema serikali imetoa kiasi cha million 210 kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule za sekondari 7 Karatu, amesema serikali imepata fedha million 76 zinazotokana na covid-19 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo.

Mh. Kayanda ametoa kiasi cha mifuko 20 kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa darasa katika shule ya Msingi Bonde la Faru linalojengwa kwa nguvu za wazazi. Mh. Kayanda ameelekeza uongozi wa shule kutumia kisima cha kuhifadhia  maji kilichojengwa kupelea bomba la maji  katika maliwato yaliyojengwa kwa ajili ya wanafunzi wa kike na wanafunzi wa kiume. Sambamba na utekelezaji huo Mh. Kayanda  ameelekeza kuwepo maliwato kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu.

Katika hatua nyingine Mh. Kayanda amehimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa ukovi-19. Amesema lazima wananchi wavae barakoa na kukaa kwa nafasi umbali wa mita moja ili kuepuka misongamano pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono. Amesema serikali kupitia wahisani na wafadhili wameleta chanjo dhidi ya ukovi-19, na amezindua zoezi hilo kwa kupokea chanjo kwa hiari. Amehimiza wananchi wenye uhitaji wa kupata chanjo kwa hiari wafike kituo cha afya Karatu, kituo cha afya Endabash, kituo cha Afya

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Lucian amewaambia wananchi wa kijiji cha Upper kitete kuanza ujenzi wa nyumba ya walimu two in one mpaka ngazi ya lenta na Halmashauri ya wilaya ya Karatu itamalizia ujenzi wa nyumba hiyo. Amesema Halmashauri itatoa lori kwa ajili ya kusomba mawe na mchanga kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya msingi Bonde la Faru. Mh.Lucian ameahidi kuwaletea jersey za mpira wanafunzi wa shule ya msingi Bonde la Faru na diwani wa Mbulumbulu Mh. Eliasi Simpa ametoa kiasi cha shilingi laki moja kwa ajili ya kununulia wanafunzi mipira. Huku Mwenyekiti wa kijiji akiahidi kuwajengea magoli ya mpira kwa ajili ya wanafunzi kujihusisha na michezo.

Naye Mwenyekiti wa Eclat Foundation (Tanzania) Mh.Toima Peter Kiroya amesema shirika linasaidia katika kuimarisha kiuchumi vikundi vya kijamii lakini wanasaidia katika miradi ya afya na miradi ya elimu kwa kushirikiana na upendo society (germany) linaloongozwa na Dr.  Freid Heimbach ambalo ndilo lilotoa fedha. Amesema  baada ya kumaliza ujenzi  wa matundu 16 kwa wavulana na matundu 16 kwa wasichana. Meza na viti 8 Ujenzi wa madarasa mawili yenye madawati 96 n ukarabati wa kisima cha kuhifadhia maji. Kwa pamoja wamekabidhiana hati  iliyosainiwa kwa pamoja  na Mkurugenzi wa Halmashauri, Mwenyekiti Eclat Foundation (Tanzania) na mwenyekiti wa Upendo society (Germany) kama ishara ya  ukamilishwaji wa ujenzi wa mradi.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...