Ndege ya mwisho ya jeshi la Marekani imeondoka Kabul, ikiashiria mwisho wa uwepo wa nchi hiyo nchini Afghanistan.
Kamanda mkuu wa jeshi la Marekani katika eneo hilo, Jenerali Kenneth McKenzie, amesema ndege ya mwisho ya C17 iliondoka Kabul ikiwa na balozi wa Marekani baada ya saa sita usiku saa za eneo hilo.
Aliongeza kuwa ujumbe wa kidiplomasia kusaidia wale ambao hawakuweza kuondoka kabla ya tarehe ya mwisho utaendelea.
Milio ya risasi ya sherehe za Taliban ilisikika baada ya ndege ya mwisho kuondoka.
Kuondoka kwa ndege hiyo ya mwisho kunaashiria kumalizika kwa vita virefu kabisa vya Marekani, na juhudi kubwa ya uokoaji ambayo ilianza tarehe 14 Agosti mara tu baada ya Taliban kuchukua nchi.
Jenerali McKenzie alisema kuwa kwa jumla, ndege za Marekani na nato ziliwaondoa zaidi ya raia 123,000 - wastani wa zaidi ya raia 7,500 kwa siku wakati huo.
Akiongea baada ya tangazo hilo, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken alizungumza huko Washington, akiita uhamishaji huo "jukumu kubwa la kijeshi, kidiplomasia na kibinadamu" na moja wapo ya changamoto kubwa kwa kazi ambayo Marekani imewahi kutekeleza.
"Ukurasa mpya umeanza," alisema. "Ujumbe wa kijeshi umekwisha. Ujumbe mpya wa kidiplomasia umeanza."
Lakini alisema kuwa Taliban ilihitaji kupata uhalali wake na itahukumiwa kwa kiwango ambacho ilitimiza ahadi na majukumu yake ya kuruhusu raia kusafiri bure kwenda na kutoka nchini, ilinde haki za Waafghan wote wakiwemo wanawake, na ilizuia vikundi vya ugaidi kutokana na kupata nafasi nchini.
Aliongeza kuwa wakati Marekani ikisitisha uwepo wake wa kidiplomasia huko Kabul, na kuhamisha operesheni zake kwenda Doha, itaendelea na "juhudi zake" za kuwasaidia Wamarekani, na Waafghan na pasi za Marekani, kuondoka Afghanistan ikiwa wanataka.
Bwana Blinken alikuwa waziri wa kwanza wa baraza la mawaziri la Biden kuzungumza kuhusu kujitoa.
Rais Joe Biden alitoa taarifa fupi kuwashukuru wale wote waliohusika katika operesheni ya uokoaji kwa siku 17 zilizopita na kusema kuwa atalihutubia taifa baadaye Jumanne.
Wakati huo huo, Marekani bado haijaelezea ripoti kwamba shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya mtu anayeshukiwa kuwa mshambuliaji wa kujitoa mhanga nchini Afghanistan liliwaua raia kadhaa, wakiwemo watoto sita na mtu ambaye alifanya kazi kama mtafsiri wa vikosi vya Marekani.
Jamaa wa watu hao walisema shambulio hilo, kwenye gari karibu na uwanja wa ndege wa Kabul, lilitokana na taarifa isiyo sahihi. Pentagon ilisema ilikuwa ikitathmini na kuchunguza ripoti hizo.

No comments:
Post a Comment