Search This Blog

Wednesday, July 14, 2021

Tozo Mpya Mafuta na Simu zaleta Ukombozi Vijijini


Tozo mpya iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia mitandao ya simu na  mafuta katika vyombo vya usafiri, zinaenda  kuwanufaisha wananchi wa vijijini kwa kufungua mtandao wa barabara vijijini.

Hayo yamesemwa leo Julai 14, 2021 na waziri wa Nchi Ofisi Rais Tamisemi (OR-TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) akikagua ujenzi wa barabara ya Santa Maria - Kabage yenye urefu wa kilomita 16 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tnganyika Mkoani Katavi.

“Nadhani Mlitusikia Mimi na Waziri wa Fedha kuwa ni jinsi gani fedha hizi za tozo ya mitandao ya simu na mafuta  zinaenda kufungua barabara vijijini. Mmemsikia Mbunge wenu kuwa hii barabara haikuwa inapitika kutoka kijiji cha Santa Maria hadi Kijiji cha Kabage ambako ni muhimu kwa uzalishaji mkubwa wa chakula hasa maza ya mpunga, lakini sasa imefunguka, “alisema Ummy.

Alieleza kuwa Serikali iliamua kufanya ubunifu baada ya kujuliza ni jinsi gani wataboresha barabara za vijijini, hivyo kubuni chanzo hicho cha tozo za simu na mafuta ambacho sasa kinaleta matokeo chanya yanayoonekana.

“Mmemsikia meneja wa Tarura Tanganyika kwamba alikuwa na bajeti ya shilingi milioni 150 tu kwa wilaya nzima ya Tanganyika, lakini sasa kwa sababu ya tozo hii mpya,bajeti yake ya maendeleo ya ujenzi wa barabara  inaenda kuongezeka mpaka shilingi bilioni moja na milioni mia tano (1.5 bilioni), “alisema Ummy.

Alisema kuwa kama milioni 150 zimeweza kujenga Km 16 za barabara ni wazi kwa bilioni 1.5 zitaenda kufungua barabara nyingi sana vijijini na kuondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi.

Aliwataka watanzania kuendelea kuchangia tozo hiyo ambayo inaenda kuleta ukombozi mkubwa vijijini.

“ Niwaombe watanzania tuendelee kumuunga mkono Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha tozo hii mpya inalipwa ili wazee wangu ninyi watanganyika mnufaike, na barabara hii ipitike kwa mwaka mzima bila shida, “ alisema Ummy.

Naye Mbunge wa jimbo la Tanganyika Mhe. Selemani Kakoko alisema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ni ukombozi  kwa wananchi kwa sababu ni kiungo muhimu kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi pamoja na usafiri baina ya kijiji cha Santa Maria na Kijiji cha Kabage.

Aidha waziri Ummy hakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kumuagiza mkandarasi kukamilisha barabara kwa muda uliopangwa bila kuongeza muda, ili wananchi waanze kufurahia matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo imedhamiria kuwakomboa wananchi wa vijijini.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...