Senegal, Umoja wa Ulaya, Marekani na wadau wengine, jana walitia saini mkataba wa kufadhili utengenezaji wa chanjo katika taifa hilo la Afrika Magharibi mjini Dakar.
Hatua hiyo imechukuliwa katika wakati ambapo kuna upungufu wa chanjo na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona, kutokana na wimbi la tatu la maambukizi lililokumba bara la Afrika ambalo limetaja kuweko kwa ukosefu wa taasisi za kutengeneza chanjo barani humo.
Taarifa ya pamoja ya serikali ya Senegal na Umoja wa Ulaya, imesema kuwa asilimia 95 ya chanjo zinazotumika barani Afrika zimeagizwa kutoka nje.
Taarifa hiyo imeongeza kwamba mkataba huo mpya wa ufadhili unanuia kuanzisha utengenezaji wa chanjo katika taasisi ya Pasteur mjini Dakar na kupunguza utegemeaji wa chanjo kutoka nje.
Aidha waziri wa masuala ya uchumi wa Senegal Amadou Hott amesema kuwa hatua hiyo itaweka msingi wa uhuru wa kimatibabu na dawa.

No comments:
Post a Comment