Kundi la nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC, pamoja na washirika wake wamekubaliana kwa pamoja kuongeza viwango vya ukomo wa uzalishaji mafuta vilivyowekwa dhidi ya nchi tano mwaka ujao na kupiga jeki uzalishaji kwa mapipa milioni mbili kwa siku ifikapo mwishoni mwaka huu. Hatua hiyo imefikiwa katika kipindi hiki dunia inapoanza kujinasua kiuchumi kutokana na janga la virusi vya corona.
Baada ya mkutano uliofanyika kwa njia ya video leo Jumapili wanachama hao wametangaza k,uwa Iraq, Kuwait, Urusi, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zitaruhusiwa kuongeza viwango vyao. Hii inamaanisha kuwa mgogoro uliokuwepo kati ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE uliokwamisha hatua ya kufikiwa makubaliano, umetatuliwa kwa sasa.
Mataifa hayo yamekubaliana kuliangalia tena suala lililoleta mvutano katika mkutano mwengine utakaofanyika mwezi Desemba.

No comments:
Post a Comment