Search This Blog

Saturday, July 3, 2021

Mbowe atoa ushauri mpya kwa Samia

 


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya katiba ili kusimamia mchakato wa kupata Katiba Mpya.


Mbowe alitoa wito huo Dar es Salaam  katika kongamano maalumu la kudai Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) likiwa na kaulimbiu ya “Katiba Mpya kwa mustakabali wa kijana wa leo na kesho.”


Wito huo unatolewa zikiwa zimepita siku chache tangu Rais Samia kuweka wazi suala la mikutano ya hadhara na Katiba Mpya kuwa visubiri kwanza ashughulike na uchumi wa Taifa.


Rais Samia alisema hayo katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.


Akizungumza wakati akifungua kongamano hilo, Mbowe alisema Watanzania wanahitaji Katiba Mpya bora na shirikishi huku akipendekeza Rais Samia aunde tume ya katiba itakayoshirikisha makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa, wasomi na wafanyabiashara.


“Tunaamini mchakato wa Katiba Mpya hauzuii ujenzi wa uchumi imara bali unaimarisha uchumi. Mambo haya hayana gharama kubwa, tunapo pa kuanzia na tutapata Katiba Mpya kabla ya mwaka 2023,” alisema mwanasiasa huyo.


Mbowe alishauri tume hiyo ichukue rejea na mapendekezo yaliyopo kwenye rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba pamoja na yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa ili kuiboresha zaidi na kutoka na Katiba bora zaidi.


Mwaka 2010, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliutangazia umma kuanza kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania.


Mchakato huo, ukaanza rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, baadaye ikatungwa sheria nyingine ya Kura ya Maoni mwaka 2013.


Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitamka kuanzishwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoanzishwa chini ya Jaji Warioba, ikaratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba ambayo kupitia uhariri wa Mabaraza ya Katiba ikapatikana Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.


Msimamo wa Serikali


Akizungumzia madai ya Chadema kuhusu Katiba Mpya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba, Amon Mpanju aliiambia Mwananchi kuwa msimamo wa Serikali tayari umeshatolewa na Rais Samia.


“Msimamo wa Serikali kuhusu mchakato wa Katiba Mpya umetolewa na Rais Samia, ambaye kwa sasa amesema ameelekeza nguvu zake katika kujenga uchumi,” alisema Mpanju.


Rais Samia aliwaomba Watanzania wampe muda ajenge uchumi kisha ataweza kuruhusu mambo mengine yaendelee ikiwemo mchakato wa Katiba Mpya na mikutano ya hadhara. Kauli ya Rais Samia imekuja ikiwa imepita miezi miwili tangu alipotoa ahadi ya kukutana na vyama vya siasa, ambapo alianza na makundi mbalimbali kwenye jamii.


“Nilisema siku ile nazungumza bungeni kwamba nitakaa na wenzangu wa vyama vya siasa tuone tunakwendaje na siasa za nchi. Ndugu zangu nchi yetu ina changamoto ya uchumi. Kuna janga la Covid-19 limetupiga,” alisema Rais Samia wakati akijibu swali.


Huku akiunganisha na swali jingine aliloulizwa na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Rais Samia alisema anajikita kujenga uchumi halafu mengine yatafuatia.


“Nimesema nakwenda kuifungua nchi kwa sababu uchumi umeshuka tunatakiwa kupandisha uchumi. Tukifungua nchi, tukiweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kazi tunaifanya vizuri,” alisema.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...