Katibu Mkuu wa Chama cha walimu Tanzania (CWT) Deus Seif,amewataka wahitimu wa Ndaki ya Ualimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao ili serikali iendelee kuipa imani sekta hiyo katika suala la usimamiaji mitihani ya taifa.
Hayo ameyasema jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la walimu tarajali na kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza pamoja na kuwaaga wanafunzi walimu mwaka wa tatu lililofanyika katika kitivo cha Walimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Bw.Seif amesema kuwa umefika wakati sasa wa nyie walimu wa Karne ya 21 kuwa
watii katika katika kazi ya ualimu ili muifanye Kada ya ualimu kuwa bora na kuvutia machoni mwa jamii.
“Msiende kuwa watu wa kuhangaika mtaani,jitumeni kitumieni chama cha walimu CWT ili muweze kusonga mbele,”amesema Seif.
Hata hivyo Seif amewataka kuitumia Benki ya Mwalimu ili kujiwekea akiba yao ya baadae kama walimu wa Karne ya 21.
”Ifike wakati Walimu mchangamkie fursa zinazotolewa kwa ajili ya walimu ambazo zitachangia kujiongeza kipato katika kada ya ualimu.
Aidha amewataka walimu nchini kuendelea kutoa maoni kuhusiana na uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya walimu Tanzania huku ikisisitiza msimamo wao ni kuipinga na kuikataa Bodi hiyo kwani imelenga kumkandamiza mwalimu badala ya kumsaidia.
Katibu Mkuu huyo amesema wakiwa Mwanza katika Mei Mosi,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan aliagiza walimu washirikishwe kutoa maoni kuhusiana na Bodi ya Kitaaluma ya walimu.
Amesema wao CWT Msimamo wao ni ashirikishwe mwalimu mwenyewe ili aweze kutoa maoni kwani kila mmoja amekuwa akiwasemewa hivyo kuna haja ya kuwa na chombo kimoja ambacho kitawasemea walimu katika mambo yao.
“Kilio cha walimu kinasemwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Tamisemi,Wizara ya Fedha na Mipango,Utumishi huyu ni mtu mmoja hata katika Soka makocha sita watawezaje kuiendesha timu Sisi kama CWT tumeotoa maoni yetu uimarishwe utendaji kazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).
“Uzuri CWT ina walimu kila sehemu naomba tushirikiane kutoa mawazo hivi ni kweli mwalimu anatakiwa aende mafunzo kila mwaka tena alipie kwa fedha yake ili kuboresha leseni yake tena mafunzo yenyewe yanagharama tunasema hapana katika hili,”amesema Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo wa Tume ya Walimu nchini (TSC), Meckitilida Kapinga, amewaasa walimu hao tarajali licha ya kuwepo kwenye karne ya kidigitali wahakikishe wanazingatia maadili ya taaluma yao badala ya kujikita kwenye mitandao ya Kijamii na kupoteza muda wa kutekeleza majukumu yao.
Awali akisoma risala Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wanafunzi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSTA) Emanuel Mwangoka amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 chama hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vyanzo vya mapato na hivyo kufanya chama kujiendesha kwa michango ya wadau kikiwemo CWT.
Pia, amesema wao kama walimu tarajali wameomba wapewe elimu kuhusiana na Bodi ya walimu Tanzania ili waweze kuifahamu utendaji kazi wao na walimu watanufaikaje na Bodi hiyo.
”kutokana na kujipambanua kurudisha chama hicho mikononi mwa wanachama wenyewe hasa kuendesha shughuli zake kwa ada za wanachama na huku huduma nyingine wakiwategemea walezi wao, hali hiyo imekuwa ngumu kuwa na fedha ya kutosha kutoka huduma zote na kujaziliza vifaa vya steshenari”amesema Mwangoka
Hata hivyo amesema kuwa jumla ya wanafunzi 232 ambao ni walimu tarajali ni wahitimu wa mwaka wa Tatu watakaokabidhiwa vyeti.



No comments:
Post a Comment