Search This Blog

Thursday, July 29, 2021

JKT Mbweni yaifunga TAMISEMI QUEENS magoli 40-39 na kutwaa ubingwa wa Netiboli


Na Mathew Kwembe, Arusha

Timu ya JKT Mbweni ya Dar es salaam imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Netiboli Ligi daraja la kwanza mwaka huu baada ya kuwafunga Mabingwa wa Kombe la Muungano la Netiboli mwaka 2019 TAMISEMI QUEENS kwa magoli 40-39 katika mchezo mkali na wa kusisimua uliofanyika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha leo.

TAMISEMI QUEENS wakiongozwa na nahodha wa timu hiyo Sophia Komba na wafungaji wake hatari Lilian Jovin na Aziza Itonye waliutawala mchezo huo mwanzo hadi mwisho wa mchezo na kuwafunika kabisa wachezaji Frida Zablon na Doritha Mbunda wa JKT Mbweni  ambao iliwabidi kutumia nguvu kuwakaba wachezaji wa TAMISEMI QUEENS.

Hadi robo ya kwanza ya mchezo inamalizika TAMISEMI QUEENS walikuwa mbele kwa magoli 10-8.

Katika robo ya pili na ya tatu TAMISEMI QUEENS waliongoza kwa magoli 19 -18 na robo ya tatu waliongoza kwa magoli 29-28

Hata hivyo Mchezo huo ulianza na dosari tangu dakika ya kwanza ya mchezo baada ya refarii namba moja Masumbuko Matata kutoka Mwanza na refarii namba mbili Enock Akyoo wa Mtwara kuamua waziwazi kuibeba timu ya JKT Mbweni.

Katika mchezo huo uliokuwa umetawaliwa na ubabe na kukamiana kwingi Mwamuzi Matata aliwaachia wachezaji wa Mbweni JKT kucheza faulo mara kwa mara hasa golikipa wa Mbweni JKT Joyce Kaila alikuwa akiwafanyia faulo za wazi wafungaji wa TAMISEMI QUEENS Lilian Jovin (GS) na Aziza Itonye (GA) jinsi alivyotaka bila mwamuzi huyo kumchukulia hatua zozote.

Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mchezaji Aziza Itonye (GA) wa TAMISEMI QUEENS ambaye mara kwa mara alikuwa akiipasua ngome ya JKT Mbweni na kulazimika kufunga magoli akiwa mbali kwa kuhofia kufanyiwa faulo na wachezaji wa JKT.  

Mchezo huo ambao ulishuhudiwa na Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni sanaa na Michezo Mhe. Paulina Gekul ambaye aliwataka CHANETA kuhakikisha katika mashindano yajayo ihakikishe inateua waamuzi bora na wenye weledi wa kuchezesha  mashindano ya ligi daraja la kwanza nchini.

Kauli ya Naibu Waziri iliungwa mkono na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt Athumani Kihamia ambaye baada ya kumalizika kwa mchezo huo alionyesha dhahiri kukerwa na Kitendo cha Mwamuzi Masumbuko Matata wa Mwanza kushindwa kuumudu mchezo huo.

“Huyu refa aliyechezesha leo kutoka Mwanza mimi siwezi kumung’unya maneno hakuchezesha kihalali na tunaweza kusema ameyatia aibu mashindano haya,” amesema Dkt Kihamia.

Dkt Kihamia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Michezo mkoa wa Arusha amesema anatarajia tukio kama hilo hataliona mwakani katika mashindano ya Ligi daraja la kwanza na badala yake aliwataka CHANETA kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanaamuliwa na marefa walio huru na uwezo.

“Kwa refa kuchezesha vile ama hana uwezo au kachukua rushwa ama timu mojawapo inamhusu, kwa hiyo mwakani tutahakikisha mambo ya namna hii hayatokei katika mkoa wetu,” alisema Dkt Kihamia.

Katika mashindano hayo Timu ya TAMISEMI QUEENS ilifanikiwa kutoa mfungaji bora wa mashindano hayo Lilian Jovin, Mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP)  Meryciana Kizenga na Mchezaji bora wa kati  wa mashindano hayo Sophia Komba.

Jumla ya timu 13 zilishiriki mashindano hayo yaliyoanza julai 19 na  kuhusisha timu tisa za wanawake na timu nne za wanaume, ambapo washindi watatu wa kwanza wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Netiboli Afrika Mashariki na timu sita za mwanzo zitashiriki katika kombe la Netiboli Zanzibar katika mashindano yatakayofanyika baadaye mwaka huu.

 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...