WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kuufungua Mnada wa mpakani wa Magena uliofungwa kwa zaidi ya miaka 20 ili uanze kufanyakazi ya biashara ya Mifugo kama ilivyokusudiwa hapo awali.
Waziri Ndaki alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya Mkoani Mara mwishoni mwa wiki, ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea kuona hali ya mnada huo na kuruhusu uanze kufanya kazi baada ya kuelezwa na kujiridhisha kuwa zile sababu zilizopelekea mnada huo kufungwa hazipo tena.
"Leo nimekuja kuufungua mnada huu wa Magena uanze kufanya kazi mara moja, ninaelekeza kuwa Halmashauri ya Mji wa Tarime na Watendaji katika ngazi ya Wizara yangu wakutane haraka ili wapange siku ambayo mnada huu utaanza kufanyakazi, na hiyo taarifa nipewe ndani ya wiki moja,"alisema Ndaki
Alisema kuwa Serikali imedhamiria kuufanya mnada huo kuwa wa kimataifa na watahakikisha wanaboresha miundombinu yote iliyochakaa ili iweze kutoa huduma nzuri na Serikali ianze kukusanya mapato yake.
"Kwa kuanzia tumetenga Milioni Mia moja hamsini kwa ajili ya kuanza kuboresha miundombinu ya mnada huu na tutaendelea kuuboresha zaidi ili uweze kuvutia watu wengi wakiwemo kutoka nchi za jirani kuja kufanya biashara hapa," aliongeza Ndaki
Aidha, aliwataka wananchi wa Wilaya ya Tarime hususan wanaoishi katika Kijiji cha Magena kuhakikisha wanautunza mnada huo ili uweze kuwa na tija kwao pamoja na nchi kwa ujumla.
Waziri Ndaki alitumia fursa hiyo pia kuwaonya wale wote wenye tabia ya wizi wa mifugo kuacha vitendo hivyo mara moja kwani ndio vilichangia hata mnada huo kufungwa, huku akisema Serikali ipo imara na imejipanga kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo ili Wafanyabiashara wa mifugo waweze kuutumia mnada huo na kufanya shughuli zao kwa amani.
"Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi wake, kufunguliwa kwa mnada huu ni katika jitihada za kuboresha maisha yenu ili kila mmoja aweze kupata maendeleo yake kupitia shughuli halali anazozifanya," alifafanua Ndaki
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alisema kufunguliwa kwa mnada huo kutatoa fursa kwa Wananchi wa Mkoa wa Mara kujiongezea kipato kupitia shughuli mbalimbali zitakazokuwa zinaendelea katika mnada huo.
Mhe. Waziri tunakushukuru kwa kutufungulia mnada huu, lakini nakuomba usiishie kuwa mnada wa mpakani tu, ni muhimu tukauboresha kwa kujenga miundombinu ya kisasa ili uwe wa kimataifa ili Serikali iweze kukusanya mapato mazuri na wananchi pia waweze kufaidika kupitia rasilimali zao," alisema Waitara
Aliongeza kuwa ni muhimu sasa operesheni inayoendeshwa na Jeshi la Polisi nchini la kupambana na wizi itumike pia kushughulika na wezi wa mifugo ili biashara hiyo iweze kwenda vizuri na kushamiri mkoani humo.
Mnada huo wa Magena ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani na ulijengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996 ambapo ulifanya kazi takriban mwaka mmoja kabla ya kufungwa kwa sababu zilizotajwa kukithiri wakati huo, ikiwemo wizi wa mifugo na sababu nyingine za kiusalama zilizopelekea Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kuufunga Mei 14, 1997.

No comments:
Post a Comment