Na John Walter-Manyara
Wajasiriamali wametakiwa kutengeneza bidhaa zenye kiwango na kuzitumia fursa za maonesho ya kibiashara kutangaza bidhaa zao na kujipatia kipato ili kupunguza tatizo la ajira nchini.
Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange akifunga maonesho ya 16 ya wajasiriamali yaliyoandaliwa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) kanda ya kaskazini yaliyofanyika katika uwanja wa Kwaraa Mjini Babati.
Twange amesema wajasiriamali wakizalisha bidhaa kwa wingi itaisaidia nchi kuwa na viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo vitaisaida serikali kuondoa wimbi la ukosefu wa ajira.
Amesema Maonesho hayo yamewap fursa Wajasiriamali kuweza kukuza soko la bidhaa zao na kuwapatia nafasi ya kukutana na wafanyabiashara wenzao kubadilishana uzoefu ambao utaendeleza sekta ya biashara nchini.
Amelipongeza shirika la SIDO kwa kuanzisha maonesho hayo katika kanda na kuwataka waendelee kuwatembelea wajasiriamali katika maeneo yao na kuwapatia elimu zaidi ili wazalishe bidaa zao kwa tija.
Katika Maonesho hayo Banda lililotembelewa na wananchi wengi ni la Wakala wa Usajili wa Biashara na leseni (BRELA) ambapo zaidi ya 100 walisajili majina ya biashara zao huku wengine wakihakiki taarifa zao.
Afisa wakala wa Usajili wa Biashara na leseni Gabriel Girangay alisema wameshiriki maonyesho hayo kwa lengo la kuwasogezea huduma karibu wananchi wa kanda ya kaskazini.
Aidha Girangay aliwashauri wadau kuacha kutumia vishoka kwani wakati mwingine watu hao wanaweka vizingiti kwa kuchelewesha kupata usajili .
Watu mbalimbali walijitokeza kwenda kuangalia maonesho hayo ambayo yamekuwa chachu ya ukuaji wa biashara ndogo ndogo zinazotoa fursa ya ukuaji wa viwanda nchini.
Moja ya biashara ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi ambayo jicho langu lilivutika kwa kasi zaidi ni ile ya Sukari Guru inayofanywa na mbunge mstaafu Jituson Virjilal, ambapo licha ya kuelezea faida lukuki za Guru katika mwili wa binadamu, alitengeneza uji uliochanganywa na sukari guru pamoja na chai ya Guru ambayo ladha yake iliwafanya wengi kupanga foleni kubwa ili kuweza kuonja Uji na chai hiyo.
Bidhaa zingine ni kutoka kwa wanawake wajasiri ambao wameamua kuacha utegemezi kutoka klwenye familia zao na waume zao na kutengeneza Pilipili za kusindika, Ubuyu na Sabuni za maji.
Maonesho hayo ya 16 ya SIDO kanda ya kaskazini mwaka 2021 yaliyoanza mei 27 na kuhitimishwa mei 31 2021 yalibebwa na kauli mbiu isemayo “Maendeleo ya viwanda nuru ya maendeleo kiuchumi”
No comments:
Post a Comment