Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
Chama kikuu cha ushirika cha RUNALI kilichopo mkoani Lindi, kimefanikiwa kuuza tani 1,864 na kilo 629 za ufuta katika mnada uliofanyika leo mjini Nachingwea.
Katika mnada huo ambao bei ya juu ilikuwa shilingi 2,307 na bei ya chini shilingi 2,280 jumla ya barua 18 zilizoandikwa na kampuni 18 kuomba kununua ufuta huo zilisomwa. Ambapo kampuni za Lenic, S.H Impex, Dizgozit, RBST , Your home na Africian zimefanikiwa kununua ufuta huo.
Katika ghala la Export lililopo Nachingwea lenye tani 801. Kampuni ya Lenic imenunua tani 260 kwa bei ya shilingi 2,295. Wakati kampuni ya S.H Impex imenunua tani 541.
Aidha kampuni za Dizgozit, RBST na Your home zimefanikiwa kununua tani 785 na kilo 813 zilizopo katika ghala la Lipande lililopo katika wilaya ya Ruangwa.
Katik ghala hilo la Lipande kampuni ya Dizgozit imefanikiwa kununua tani 150 kwa bei ya shilingi 2,303, kampuni ya RBST tani 500 kwa shilingi 2,295 na kampuni ya Your home tani 135 na kilo 813 kwa shilingi 2,280.
Licha ya kampuni hizo kununua katika maghala hayo, lakini pia kampuni ya Your home kwa mara nyingine imefanikiwa kununua tani 77 kati ya tani 277 na kilo 259 zilizopo katika ghala la umoja wilayani Liwale kwa shilingi 2,285. Ambapo kampuni ya Afrisian katika ghala hilo imenunua tani 200 kwa bei ya shilingi 2,307 kila kilo moja.
Akizungumza katika mnada huo wa kwanza msimu wa 2021 kwa RUNALI na wanne kwa mkoa wa Lindi, katibu tawala wa wilaya ya Nachingwea, Omari Mwanga alizitaka benki na RUNALI zihakikishe wakulima wanalipwa kwawakati.
Alisema kuchelewesha malipo ya wakulima kunasababisha wauze ufuta wao kwa walanguzi. Kwahiyo wakilipwa mapema kutazifanya taasisi hizo kushiriki kikamilifu kuzuia wakulima hao wasidhulumiwe na walanguzi.
Mwanga alisema ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo imekuwa ikipokea malalamiko mengi ya wakulima. Malalamiko mengi kati ya hayo ni kucheleweshwa malipo yao.
Nae kaimu mrajisi msaidizi wa mkoa wa Lindi, Richard Zengo aliwataka wanunuzi wahakikishe wanawalipa wakulima ndani ya siku nne tangu siku ya mnada, watoe mizigo yao kwawakati toka maghalani na vyama vya msingi vipeleke benki taarifa za wakulima kwawakati.
Kwaupande wao wakulima Hamis Chitanda( Chininje) Amthom Lalo na Rajab Rashid( Maliyamungu) walisema bei hizo ni nzuri zilinganishwa na bei za msimu uliopita. Huku wakiahidi kuendelea kulinda ubora wa zao hilo ili bei ziongezeke.

No comments:
Post a Comment