Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzungumza na wanawake zaidi ya 10,000 mkoani Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amesema hayo leo Juni 6, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Mtaka amesema Rais Samia atazungumza na wanawake wa mkoa huo kwa niaba ya wanawake wote nchini katika ukumbi wa Jakaya Convertion, Jumanne ya Juni 8, 2021. Hata hivyo, ajenda ya mazungumzo hayo haikuwekwa wazi.
Amesema wanawake kwa uwakilishi wao wa makundi kutoka wilaya za Dodoma na maeneo ya karibu wamepewa mwaliko wa kushiriki kwenye mkutano huo.
"Kwa uchache pia kama makundi ya wabunge wanawake bila kujali uko chama gani, madiwani na makundi kama wajasiriamali, mama ntilie na kila aina ya wanawake watapata nafasi ya kuwakilishwa na wenzao," amesema.
Aidha, Mtaka amewakaribisha waandishi wa habari kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa mkuu wa mkoa huo kufanya kazi naye kwa ushirikiano.

No comments:
Post a Comment