Search This Blog

Tuesday, June 8, 2021

Mbeya yaanza vyema michuano ya UMITASHUMTA


Na Mathew Kwembe, Mtwara

Timu ya soka ya mkoa wa Mbeya imeyaanza vyema michuano ya UMITASHUMTA mwaka huu baada ya kuifunga timu ya soka ya mkoa wa Morogoro kwa magoli 3-1 katika mojawapo ya michezo miwili ya ufunguzi iliyofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilifungana kwa goli 1-1 ambapo kipindi cha pili timu ya mkoa wa Mbeya ilicharuka na kufunga magoli mengine mawili ambayo yalifungwa na wachezaji Omary Enock, Samson Mashaka na Enjobatt Said.

Kufuatia ushindi huo, kocha wa timu ya soka wavulana kutoka mkoa wa Mbeya Mwalimu Wycliff Kolimba ametamba kuwa timu yake imejiandaa kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu.

Tofauti na mwaka 2019, ambapo timu yake ilitolewa katika hatua ya makundi, mwaka huu, Mwalimu Kolimba ambaye anafundisha shule ya msingi Muungano mjini Mbeya ameahidi kulibeba kombe hilo licha ya timu yake kukabiliwa na ushindani kutoka timu ngumu katika kundi lake ikiwemo bingwa mtetezi Geita.

Timu nyingine zinazounda kundi hilo ni pamoja na wenyeji Mtwara, Lindi, Kigoma na Morogoro.

Kocha huyo amesifu kuwepo kwa michuano hiyo kwani itasaidia kuibua vipaji vya watoto hasa wa umri wa miaka 12 hadi 14 ambavyo isingekuwa kuwepo kwa mashindano hayo vingeishia mtaani tu.

Michuano hiyo itaendelea kesho katika viwanja mbalimbali vya chuo cha ualimu Mtwara.

Caption: Baadhi ya wachezaji na mashabiki wa timu ya soka ya mkoa wa Mbeya  wakiwa na furaha baada ya timu yao kuifunga timu ngumu ya mkoa wa Morogoro magoli 3-1 katika uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara

Winga machachari wa timu ya soka wavulana ya mkoa wa Mbeya Geshon Lameck ( jezi namba 11) akijaribu kumtoka beki wa timu ya mkoa wa Morogoro Salmin Rajab (jezi namba 12) wakati wa mechi za ufunguzi wa michuano ya UMITASHUMTA iliyofanyika katika viwanja vya Nangwanda mjini Mtwara leo.

Mabeki wa timu ya soka ya mkoa wa Morogoro (jezi nyekundu wakiwa katika jitihada za kuwazuia washambuliaji hatari wa timu ya mkoa wa Mbeya Geshon Lameck (jezi namba 11) na Omary Enock (jezi namba 14) katika mojawapo ya misukosuko katika lango la mkoa wa Morogoro.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...