Jeshi la Israel limewauwa Wapalestina sita leo, akiwemo mmoja ambaye inasemekana alijaribu kumdunga kisu mwanajeshi wa Israel.
Vifo vya watu hao vimethibitishwa na wizara ya afya ya mamlaka ya Wapalestina mjini Ramallah, na shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema makabiliano baina ya Wapalestina na jeshi la Israel katika Uganda wa Gaza yamewajeruhi watu zaidi ya 100.
Hayo yanajiri kukiwepo hali ya sintofahamu juu ya kinachoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas, huku baadhi ya ripoti zikisema pande hizo mbili zimeendelea kushambuliana. Israel imesema hivi leo kuwa imepeleka ndege 160 za kivita katika ukanda wa Gaza kuharibu mfumo wa njia za chini ya Ardhi unaoendeshwa na Hamas.
Msemaji wa jeshi la Israel Kanali Jonathan Conricus amesema ingawa vifaru vinasaidiana na operesheni ya angani dhidi ya ukanda wa Gaza, hakuna mwanajeshi wa Israel aliyeingia katika ukanda huo kama ilivyoripotiwa awali.

No comments:
Post a Comment