Na Hamisi Nasri,MASASl
WAKAZI wa wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wamehimizwa kujikita zaidi katika matumizi ya majiko sanifu ya kuni yanayotumia kuni na mkaa kwa kiwango kidogo ili kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira wilayani humo ikiwemo ukataji miti hovyo.
Wito huo ulitolewa jana mjini Masasi na mtaalamu wa nishati endelevu na mabadiliko ya tabia nchi kutoka Taasisi ya kuendeleza nishati asilia Tanzania (TaTEDO) Shima Sago alipokuwa akikabidhi majiko sanifu mawili kwa uongozi na wanafunzi wa chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi (FDC) wanafunzi wa chuo hicho ili wawe mabalozi kwa wengine.
Sago alisema kuwa licha ya kutoa majiko hayo sanifu na kutoa elimu katika chou hicho cha maendeleo ya wananchi Masasi wamekuwa pia wakifanya programu kama hizo katika mikoa mingine ikiwemo Lindi na Ruvuma kwa kanda ya kusini kwa kushirikiana na wafadhili wakiwemo,WWF na shirika la maendeleo la Sweden(SIDA)
Alisema iwapo jamii ikianza kubadilika na kutumia majiko sanifu ya kuni ambayo hutumia kuni chache kupika chakula kingi kwa muda mfupi itasaidia hata kupunguza uharibifu mazingira ikiwemo ukataji miti hivyo.
Sago alisema majiko hayo yanauwezo wa kupunguza matumizi ya kiwango cha nishati ya kuni kwa asilimia 66 na kwamba yanasaidia hata kuwa katika hali ya afya salama kwa sababu hayana moshi na joto wakati matumizi yake.
“Ubora wa majiko haya unasaidia hata kumuepusha anayetumia kuathirika kiafya kwa sababu hayana moshi na hayana joto kwani wapishi wengi ambao hawatumii majiko kama haya wamekuwa wakilalamika matumizi ya majiko ya kutumia kuni nyingi yanawathiri kiafya,” alisema Sago
Alisema katika ukanda wa Mtwara na Ruvuma taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya utoaji elimu ya kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa wingi badala yake jamii inapaswa kuanza kutumia majiko hayo bora ya kuni chache.
Alisema kwa hali ilivyo hivi sasa matumizi ya majiko kwa kutumia mafiga matatu sio rafiki kwa sababu majiko hayo yamekuwa yakitumia kuni na mkaa kwa kiwango kikubwa hali inayochangia uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti hivyo.
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Masasi,ambaye pia ni afisa mazingira wa halmashauri hiyo.Kulwa Maige amewapongeza TaTEDO,WWF na kwa kuwapatia elimu na msaada wa majiko sanifu bora wanafunzi wa chou cha maedeleo ya wananchi Masasi(FDC)
Naye mratibu wa mpango wa kuleta mabadiliko kutoka taasisi ya WWF wilaya ya Masasi Daniel Mvela alisema kwa sasa wanaratibu programu ya miaka mitano katika kuhimiza jamii kuweza kunufaika na uhifadhi wa maliasili pamoja na mazingira.
Alisema WWF imekuwa ikifanya kazi na TaTEDO na wadau wengine wa maendeleo na jamii kwa ujumla katika kuwaelimisha wananchi kushiriki kikamili kulinda mazingira na rasilimali katika uhifadhi.
Akisoma taarifa fupi ya matumizi ya nishati ya kuni katika chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi, kaimu mkuu wa chuo hicho, Alfred Mwakagenda alisema awali kabla ya kupewa majiko hayo TaTEDO wakitumia mizigo ya kuni 960 kwa mwezi ila sasa watatumia kuni chache.

No comments:
Post a Comment